Na. Happiness Sam - Mbeya


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), leo Desemba 17, 2025 amefanya ziara katika Hifadhi ya Taifa Kitulo kwa lengo la kujionea shughuli za utalii huku akiagiza kuimarishwa kwa huduma na masoko ya utalii ili kuongeza idadi ya wageni wa ndani na nje ya nchi jambo ambalo litachagiza maendeleo ya utalii wa nyanda za juu kusini.

“Ni lazima tuimarishe huduma na masoko ya utalii hapa Kitulo ili kufungua fursa za kiuchumi na ajira kwa wakazi wa nyanda za juu kusini, kwa lengo la kuondoa utegemezi wa utalii katika kanda moja na kukuza pato la Taifa kupitia rasilimali tulizonazo kwa kanda ya kusini,” alisisitiza Waziri Kijaji.

Katika kuhakikisha azma hiyo ya kukuza utalii inafanikiwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Kusini, Godwell Meing’ataki, alieleza namna hifadhi hiyo inavyozingatia misingi imara ya uhifadhi endelevu, huku mkazo ukiwekwa katika ulinzi wa mifumo ya ikolojia, usimamizi wa maliasili na ushirikiano na jamii zinazoizunguka hifadhi hiyo.

Kamishna Meing’ataki aliongeza kuwa TANAPA inaendelea kuboresha huduma kwa watalii ikiwemo miundombinu ya ndani ya hifadhi, maeneo ya malazi na utoaji wa elimu kwa wageni, hatua inayolenga kuongeza siku za kukaa kwa watalii ndani ya hifadhi na kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za utalii.

Katika ziara hiyo, Dkt. Kijaji aliambatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande (Mb), Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Nkoba Mabula, pamoja na viongozi wengine wa wizara na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA). Pia Waziri Kijaji alipata fursa ya kutembelea maeneo ya vivutio vya asili katika hifadhi hiyo.

Hifadhi ya Taifa Kitulo ni miongoni mwa hifadhi maarufu nchini kutokana na utajiri wa maua ya asili, uwepo wa wanyamapori, maporomoko ya maji na mandhari ya kipekee ya nyanda za juu, hali inayoiweka katika nafasi ya kipekee kwenye kukuza utalii endelevu na kuongeza mapato ya Taifa.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...