Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini, Mhe. Bishwadip Dey, katika ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam, tarehe 06 Desemba, 2025.

Mazungumzo hayo yamezingatia maeneo ya ushirikiano zaidi kati ya Tanzania na India, kwa lengo la kuimarisha diplomasia ya kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Kombo ameishukuru Serikali ya India, kupitia ubalozi wake nchini, kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya afya, ikiwemo kambi maalum ya kugawa viungo bandia kwa Watanzania waliopoteza viungo, iliyofanyika hivi karibuni kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Ubalozi wa India nchini.

Mheshimiwa Kombo ameiomba India kuendelea na kampeni hizo, ikiwemo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Kilimanjaro Christian Medical Center (KCMC), ili kuwafikia watu wengi zaidi waliopatwa na ulemavu baada ya kupoteza viungo vyao.

Naye Balozi wa India nchini, Mhe. Bishwadip Dey, ameonesha azma ya India ya kuongeza ushirikiano na Tanzania katika sekta za kilimo (mbaazi/pigeon peas), maji, mafunzo kwa madaktari na wafamasia, ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu vya India, biashara na uwekezaji, kwa lengo la kuimarisha diplomasia ya watu kwa watu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mataifa haya mawili.

Aidha, Balozi Bishwadip Dey amesisitiza umuhimu wa Tanzania na India kushirikiana katika kuelimisha wananchi kuhusu mafanikio ya miradi ya maendeleo na thamani ya uhusiano wa nchi hizi kimataifa, ili kuviendeleza kwa vizazi vijavyo.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...