NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewaalika wadau na watengenezaji wa bidhaa mbalimbali ndani na nje ya nchi kutembelea maktaba ya shirika hilo ili kupata na kujifunza viwango vinavyohifadhiwa, hatua inayolenga kuwajengea uelewa mpana kuhusu mahitaji ya viwango kwa bidhaa zao.

Wito huo umetolewa leo, Desemba 16, 2025, jijini Dar es Salaam na Mkutubi wa Maktaba ya TBS, Clavery Chausi, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya shirika hilo.

Amesema matumizi ya huduma za maktaba yatawawezesha watengenezaji kuongeza ushindani wa bidhaa zao katika soko la ndani na la kimataifa, pamoja na kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokubalika kulingana na matakwa ya viwango.

Chausi ameongeza kuwa maktaba hiyo iko wazi pia kwa watafiti na wanazuoni wanaohitaji taarifa na rejea kwa ajili ya tafiti zao na masomo ya juu, hususan katika masuala yanayohusu ubora wa bidhaa na uandaaji wa viwango, jambo litakalosaidia kukuza maarifa na ubunifu katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wake, Afisa Viwango wa TBS, Filbeta Magidangapp, amesema ushiriki wa wadau ni nguzo muhimu katika kuhakikisha viwango vinavyoandaliwa vinazingatia mahitaji halisi ya watumiaji na wazalishaji, vinakuwa rahisi kutekelezeka, na vinakidhi matakwa ya soko katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Magidanga ameeleza kuwa wananchi na wadau wana fursa ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uandaaji wa viwango kwa njia mbalimbali, ikiwemo kuwasilisha mahitaji ya uandaaji wa viwango kwa bidhaa ambazo bado hazijapangiwa viwango, kutoa maoni katika hatua tofauti za uandaaji wa viwango vinavyoendelea, pamoja na kupendekeza maboresho au uhuishaji wa viwango vilivyopo tayari.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...