Na Pamela Mollel, Arusha

Mkoa wa Arusha umefungua ukurasa mpya katika sekta ya afya baada ya kuzinduliwa ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Huduma za Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru, mradi unaofadhiliwa na kampuni ya Spanish Tiles.

Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la kituo hicho, Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema ujenzi huo ni hatua kubwa itakayobadili maisha ya wagonjwa wa saratani kutoka Arusha na mikoa jirani, waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.

Mhe. Mchengerwa ameiagiza Wizara ya Afya kupitia Katibu Mkuu wake Dkt. Seif Shekalaghe kuhakikisha kuwa ndani ya wiki mbili zijazo, vifaa tiba muhimu vinafikishwa hospitalini hapo ili wananchi waanze kupata huduma mara moja.

Ameipongeza kampuni ya Spanish Tiles, chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji Bw. Bobby Chadha, kwa kuonesha uzalendo na moyo wa kuwekeza katika maisha ya Watanzania, akisema mchango huo unaunga mkono juhudi za Serikali katika kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi.

Waziri huyo ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji wengine kuiga mfano wa Spanish Tiles kwa kuwekeza kwenye sekta ya afya, akisisitiza kuwa ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali ni nguzo muhimu katika kupunguza gharama za matibabu na kuokoa maisha.

Kwa upande wake, Bw. Bobby Chadha ameishukuru Serikali kwa mazingira mazuri ya ushirikiano na kusisitiza kuwa kampuni hiyo imeguswa na wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuimarisha huduma za afya, hasa katika mikoa inayopokea idadi kubwa ya watalii kama Arusha.

Ameeleza kuwa Spanish Tiles iko tayari kushirikiana zaidi na Serikali katika miradi mingine ya kijamii, hususan kusogeza huduma za saratani katika maeneo mengine yenye uhitaji mkubwa.

Kukamilika kwa kituo hicho kunatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa gharama na usumbufu kwa wagonjwa waliokuwa wakilazimika kusafiri hadi Hospitali ya Ocean Road au hata nje ya nchi, hatua itakayoboresha ustawi wa kiuchumi na kijamii wa wananchi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...