Na Nasra Ismail, Geita.
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita leo Januari 30,2026 limefanya Mikutano wake Maalum kujadili na kupitisha rasimu ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Akiwasilisha rasimu hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri uliopo Nzera Bi Sarah Yohana ambaye ni Afisa Mipango Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ameliomba baraza hilo kupokea mpango wa bajeti ya mwaka 2026/27 yenye jumla ya Shilingi Bilioni 112.8.
Aidha Afisa Mipango Bi Sarah Yohana amelieleza baraza hilo kuwa Bajeti hiyo imezingatia mapendekezo na ushauri uliotolewa na kamati za kudumu za Halmashauri pamoja na Baraza la Wafanyakazi kwa ajili ya kuleta ufanisi katika usimamizi na utekelezaji wa bajeti hiyo.
Bajeti hiyo inajumuisha fedha za mapato ya ndani Kiasi cha Shilingi Bilioni 15.8, Ruzuku ya Mishahara Bilioni 78.9, Ruzuku ya matumizi mengineyo Bilioni 1.5 na Ruzuku ya miradi ya maendeleo Bilioni 16.5
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri Dkt Modest Buchard amelipongeza baraza Hilo kwa namna lilivyoidhinisha mpango huo wa bajeti 2026/2027.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Geita Komredi Barnabas Mapande amelieleza Baraza hilo kuwa ili miradi ya maendeleo ikamilike hakuna budi kuweka bidii katika ukusanyaji wa mapato.
" Ili miradi iende lazima tukusanye mapato kwa kila mmoja kutekeleza wajibu wake kwa kushirikiana Madiwani na wataalam ambao ni watendaji katika Halmashauri" Amesema Komredi Mapande.
Pamoja na hayo, Komredi Mapande ameongeza kuwa ili kufanya kazi vizuri lazima Halmashauri iwe na utulivu na kuwataka Watumishi wa Halmashauri kusimama katika nafasi zao ili kuendana na kasi ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye Katibu Tawala Wilaya ya Geita Bi Lucy Beda amelipongeza baraza Hilo kwa kuwa na kikao kizuri kwa kupitisha Mpango wa Bajeti 2026/27.
Bi Lucy Beda amesema Halmashauri ya Wilaya ya Geita inavyo vyanzo vingi vya mapato hivyo Halmashauri iendelee kuongeza udhibiti katika ukusanyaji wa mapato ili kufikia adhma ya serikali kufanikisha miradi ya maendeleo.
“Tunalojukumu kubwa la kuongeza usimamizi na ukusanyaji wa mapato” Amesema BI Lucy beda.
Katibu Tawala huyo ameongeza kwa kusema Halmashauri iendelee kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano ili kusonga mbele.
Akihitimisha kikao cha Bajeti katika Baraza Hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Jumanne Misungwi amesema madiwani na wakuu wa idara wamejipanga kuongeza mapato ya Halmashauri kwa kufata mikakati waliyo azimia.
Mhe Misungwi amewataka Wataalam kuongeza kasi katika ukusanyaji wa mapato na kufanya kazi kwa bidii ili kuisadia Serikali.
Vilevile Mhe Misungwi ameishukuru Serikali inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu kwa kazi nzuri anazozifanya na kusema Halmashauri itaendelea kufanya kazi kuendana na kasi yake kuleta maendeleo chanya.












Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...