
MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imezindua Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa Kampuni ya Africa Pension Fund Limited (APEF) unaoitwa Ziada Fund.
Akizungumza leo Januari 26,2026 jijini Dar es Salaam,Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo CPA Nicodemus Mkama, amesema uzinduzi wa Mfuko huo ni baada ya idhini iliyotolewa na mamlaka hiyo baada ya Africa Pension Fund Limited kukidhi matakwa ya Sheria.
Hata hivyo amesema uzinduzi wa mfuko huo ni tukio la kihistoria ambalo lina mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa masoko ya mitaji na uchumi kwa ujumla hapa nchini.

“Ziada Fund ni mfuko wa uwekezaji wa pamoja wenye ubunifu wa kuwekeza katika Masoko ya Mitaji na Masoko ya Fedha; na ambao Unatoa Bima ya Maisha kwa wawekezaji.”
Aidha amesema sekta ya masoko ya mitaji hapa nchini ina wadau wengi wanaounga mkono utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya masoko ya mitaji inayoakisiwa kwa uanzishaji wa bidhaa mpya na bunifu, zinazotoa wigo mpana kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa kushiriki katika masoko ya mitaji hapa nchini.

“Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli katika masoko ya mitaji zinafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta uwazi na haki kwa washiriki wote.
“Pamoja na jukumu la kusimamia na kuendeleza masoko ya mitaji hapa nchini, CMSA pia ina jukumu la kuidhinisha maombi ya kuanzisha bidhaa mpya katika masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.”





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...