Na Diana Byera_Bukoba.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Bukoba kuhakikisha wanashiriki vyema zoezi la kuhakikisha watoto wote wanaotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza, elimu ya awali na darasa la kwanza wanaenda shuleni kabla ya daftari la usajili kufungwa.

Kupitia kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026, amesema anasikitishwa na baadhi ya wazazi na walezi ambao hawajatekeleza agizo la watoto wao kuanza mwaka wa masomo tangu shule zilipofunguliwa Januari 13 mwaka huu, huku akikemea kushuka kwa maadili kwa baadhi ya wanafunzi.

“Madiwani tujitahidi sana kupitia katika maeneo ya vitongoji vyetu, kupitia kwa wazazi, tuone namna ya kuondoa changamoto ya watoto kutoenda shuleni. Lakini hali ya maadili kwa watoto wetu hairidhishi.

Kuna mimba nyingi katika umri mdogo kuanzia shule za msingi, na kuna viashiria vingi vya watoto wa sekondari katika Halmashauri yetu kuvuta bangi. Naomba madiwani tuuokoe uzazi na tukemee sana ili kurudisha maadili,” amesema Sima.

Kupitia kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bukoba ametoa takwimu halisi za wanafunzi ambao mpaka sasa wamerepoti kidato cha kwanza na elimu ya msingi, ambapo elimu ya awali wanafunzi waliokadiriwa kujiunga ni 10,261, waliosajiliwa kujiunga mpaka sasa ni 6,761 sawa na asilimia 66.

Wanafunzi wa darasa la kwanza waliotarajiwa kujiunga ni 10,055, na waliosajiliwa mpaka sasa ni 6,812 sawa na asilimia 68, huku kidato cha kwanza waliochaguliwa kujiunga ni 5,245 na mpaka tarehe 29 Januari walijiunga ni asilimia 85.

Madiwani wa Halmashauri hiyo, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati inayoshughulikia masuala ya elimu, Severine Kijoma, wamesema watahakikisha wanashirikiana na uongozi kuanzia ngazi za vijiji na vitongoji ili watoto wote wenye sifa za kuwa shuleni wawepo shuleni kabla ya daftari kufungwa.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...