Mwamvua Mwinyi, Rufiji Januari 30, 2026
MKUU wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba, ameagiza wafugaji wote wilayani humo kuanza usajili upya kuanzia Februari mwaka huu, ikiwa ni hatua ya kuimarisha utekelezaji wa mpango wa ranchi ndogo unaolenga kudhibiti migogoro kati ya wakulima na wafugaji pamoja na kupata takwimu sahihi za mifugo.

Komba alisema kuwa usajili huo utahusisha taarifa muhimu zikiwemo jina la mfugaji, namba ya kitalu pamoja na idadi ya mifugo, akisisitiza kuwa mfugaji yeyote atakayebaki nje ya mfumo huo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

“Mpaka Oktoba 2025 tulikubaliana na wafugaji kwamba ifikapo Januari 2026 wote wawe wamehamia kwenye ranchi ndogo ili kuwezesha kupata idadi halisi ya mifugo, na atakayebaki nje atachukuliwa hatua,” alibainisha Komba.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alieleza, hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa ranchi ndogo ambao Mkoa wa Pwani una zaidi ya ranchi ndogo 800, mfumo unaowawezesha wafugaji kumiliki maeneo rasmi ya malisho, kutambua mifugo na kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Akizungumza katika ranchi ndogo ya Chumbi C wilayani Rufiji, , alisema wafugaji wanapaswa kufuga kwa njia za kisasa huku wakulima wakilima kwa tija, akibainisha kuwa mkoa una mipango madhubuti ya matumizi bora ya ardhi.

Kunenge alieleza , Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatamani kuona wafugaji na wakulima wakifanya shughuli zao kwa njia za kisasa, kitaalamu na kwa tija ili kuinua maisha yao kiuchumi.

“Ardhi haiongezeki, watu wanaongezeka na shughuli za kiuchumi zinaongezeka. Hivyo, ardhi kidogo tuliyonayo itumike kwa utaalamu ili kuleta manufaa ya kiuchumi,” alisisitiza Kunenge.

Aidha, Kunenge alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Rufiji kwa mipango na usimamizi mzuri uliosaidia kudhibiti migogoro kati ya wakulima na wafugaji wilayani humo.

Kwa upande wake, mfugaji Lisesi Kundugu aliipongeza Serikali kwa mpango wa ranchi ndogo, akisema umechangia kupunguza ufugaji holela pamoja na changamoto za upatikanaji wa malisho na maji.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...