WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka wizara zinazohusika na masuala ya ajira zisimamie kikamilifu utekelezaji wa sheria zinazotaka kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania zisifanywe na wageni isipokuwa zile zinazohitaji utaalamu ambao nchi inaupungufu.

 Vilevile, Waziri Mkuu amekemea tabia ya baadhi ya wenye nyumba kumpangisha raia mmoja wa kigeni na kumruhusu mpangaji huyo apangishe watu wengine ndani ya nyumba hiyo jambo ambalo ni hatari kwa usalama na pia halina tija kibiashara.

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo Jumatano, Januari 14, 2026 alipofungua Kikao cha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta kujadili fursa za ajira ndani na nje ya nchi.

Agizo hilo linalenga kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania kufuatia kuwepo kwa wimbi kubwa la wageni kufanya kazi au biashara ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania na kuliwezesha Taifa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa ajira.

“…Kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania ziachwe wafanye, si kuruhusu wageni wafanye. Tusioneane aibu kama tumefungua milango au kulegeza wataalamu wafuatilie. Wageni wafanye kazi za kitaalamu ambazo nchi ina uhaba wa wataalamu.”

 Amesema kuwa ni lazima wataalamu wa ndani wasimamie sheria ipasavyo na kama kuna maeneo yanayokwamisha wayabainishe na yafanyiwe marekebisho. “Hatuwezi kuleta watu wanaokuja kufanya kazi ambazo Watazania wanaziweza.” 

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa Watanzania kuwa na wivu na nchi yao kwa kutoruhusu baadhi ya vitu kufanyika, ambapo alitolea mfano suala la wenye nyumba kumpangisha raia moja wa kigeni ambaye naye analeta wenzake wengi katika nyumba hiyo hiyo.

“Watanzania tuwe na wivu na nchi yetu, mfano mtu anamkodishia nyumba mgeni kwa dola 5,000 kwa mwaka na kisha mgeni huyo anawaleta wenzake 60 na anawakodisha dola 500 hapo Mtanzania anapata hasara, hii si sawa hata kwa usalama.”

Waziri Mkuu amewaagiza wahusika wafuatilie suala hilo la makazi ili wakae katika utaratibu ulio rasmi. “Eneo hili liangaliwe wageni wanalundikana na kufanya kazi ambazo Watanzania wangeweza kufanya, hatuwezi kuruhusu hili tunataka wawekezaji.”

Hivyo, Waziri Mkuu ameziagiza wizara zinazohusika zifuatilie suala hilo, pamoja na kuwasisitiza wasimamie utekelezwaji wa sheria kwa sababu kila nchi ina sheria zake na Tanzania inatekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria.

Amesema sheria zimetungwa ili kusaidia kujenga kampuni za Watanzania na kuzikuza, hivyo wizara zinazohusika zihakikishe hazisajili kampuni za kigeni kabla ya kuzifanyia uchunguzi wa kina kwa sababu baadhi ya taarifa zinazowasilishwa si sahihi.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...