Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Ruvuma Alan Njiro, amewataka wananchi kuacha kabisa tabia ya kukata miti au kufanya shughuli zozote karibu na miundombinu ya umeme wakati umeme ukiwa unawaka ni hatari na inaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo, kwani TANESCO hulazimika kukata umeme kwanza kabla ya kufanya kazi yoyote kwenye nguzo au transfoma ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza na wakazi wa Gumbiro, Halmashauri ya Madaba, Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Njiro amesisitiza kuwa umeme ni hatari na unahitaji tahadhari kubwa wakati wote, amesema ajali nyingi za umeme husababishwa na uzembe au uelewa mdogo wa wananchi juu ya matumizi salama ya umeme.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kutumia muda wao kuwakumbusha watoto kuwa umeme ni hatari na unaweza kuua, hivyo hawapaswi kuchezea nyaya za umeme, hasa zile zilizoanguka chini au nyaya za “stay” zinazochimbiwa ardhini, ameonya kuwa kuchezea miundombinu hiyo kunaweza kusababisha majanga yanayoweza kuepukika endapo tahadhari zitazingatiwa.
Njiro pia ametoa wito kwa wakulima ambao mashamba yao yana nguzo za umeme kuacha mazoea ya kulima karibu na nguzo hizo au kushika nyaya za umeme, amesema kufanya hivyo kunahatarisha maisha yao, na amesisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari ili kuhakikisha wanakuwa salama muda wote.
Ameongeza kuwa endapo mwananchi anahitaji kukata miti katika eneo lenye nguzo au nyaya za umeme, anapaswa kuwasiliana na TANESCO ili wataalamu wafike kushusha nyaya na kuzima umeme kabla ya zoezi hilo kufanyika, Kwa maeneo hatarishi zaidi, amesema TANESCO hulazimika kukata miti hiyo wenyewe ili kuzuia ajali na kulinda usalama wa wananchi.
Katika hatua nyingine, Njiro amewakumbusha wananchi kuwa maombi ya kuunganishiwa umeme ni bure, na gharama ya kupata umeme vijijini ni shilingi elfu 27 tu, amesisitiza kuwa malipo hayo hufanyika kupitia namba ya kumbukumbu ya malipo na si kumpa mtu fedha mkononi, akiwataka wananchi kuwa waangalifu ili kuepuka utapeli.
TANESCO Mkoa wa Ruvuma imewahimiza wananchi kuzingatia taratibu za usalama wanapohitaji kukata miti karibu na miundombinu ya umeme kwa kushirikiana na TANESCO, Ushirikiano huo utasaidia kulinda maisha ya wananchi, kuepusha majanga yasiyo ya lazima na kuhakikisha miundombinu ya umeme inalindwa kwa manufaa ya jamii nzima.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...