Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali imejizatiti kuhakikisha Sekta ya Uchukuzi inaimarika ili kuliweka Taifa kwenye nafasi nzuri ya ushindani wa kibiashara, kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kukuza mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa.

 Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Jengo la Viongozi Mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Amesema pamoja na ujenzi wa jengo hilo, Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kikamilifu kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kisekta kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa na Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2025).

 Makamu wa Rais amesisitiza kwamba, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali katika Viwanja vya Ndege, huduma za usafiri wa barabara, usafiri majini na usafiri kwa njia ya reli. Halikadhalika amesema, Serikali itaendelea na uboreshaji wa  huduma za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa lengo  kuboresha usafiri wa ndani, kuunganisha Tanzania na nchi nyingine, kupunguza gharama za usafirishaji na kuimarisha uchumi wa Tanzania na biashara za kimataifa.

Vilevile, Makamu wa Rais amesema ili kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji, Serikali imedhamiria kuunganisha huduma za Sekta ya Uchukuzi, kama vile uunganishaji wa huduma za Viwanja vya Ndege,  usafiri wa barabara, maji na reli. Mathalan, mradi wa kimkakati unaoendelea wa ujenzi wa barabara za Mwendokasi (BRT) kati ya eneo la Posta na Gongo la Mboto utaunganishwa na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere ili kurahisisha huduma za usafiri katika jiji la Dar es Salaam.

 Hali kadhalika, hatua za utekelezaji zinaendelea ili kuhakikisha huduma za reli zinaunganishwa na viwanja vya Ndege vya kimataifa, hususan Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro.

 Aidha, Makamu wa Rais amesema Jitihada hizo kubwa zinazofanywa na Serikali zinalenga kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi kitaifa na kikanda. Ameongeza kwamba, hiyo inatokana na fursa na faida za kijiografia za Tanzania, ambayo ni lango kuu la biashara la nchi zaidi ya nane  zilizopo Kusini, Mashariki na Kati ya Bara la Afrika, na kiunganishi cha Bara la Afrika na nchi za Mashariki ya Kati na Mbali.

 Makamu wa Rais amesema, dhamira ya Serikali ni kuendeleza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo, ujenzi wa reli ya kisasa  kwa vipande na maeneo yote yaliyobaki kuelekea Tabora, Mwanza na Kigoma hadi Musongati (Burundi), uboreshwaji wa Bandari ya Dar es Salaam na Bandari nyingine za kimkakati za Tanga, Mtwara, Kisiwa Mgao, Mbamba Bay, Kigoma na Bagamoyo, uboreshaji wa reli ya TAZARA, ujenzi na ukarabati wa barabara za lami zinazounganisha Tanzania na nchi za jirani.

 Pia, Makamu wa Rais amesema uwekezaji wa Serikali katika Sekta ya Uchukuzi umeleta manufaa makubwa. Mathalan, mchango  wa Sekta ya Uchukuzi katika Pato la Taifa uliongezeka kutoka 7.2% (2023) hadi 7.5% (2024). Kasi ya ukuaji wa Sekta ya Uchukuzi iliongezeka kutoka 4.1% (2023) hadi 4.2% (2024) na katika kipindi cha hivi karibuni  ilikua kwa wastani wa 5.4%.

 Makamu wa Rais ametoa rai kwa kwa Watanzania wote kutambua wajibu wa kuilinda na kuitunza miundombinu inayoendelea kuwekezwa na Serikali kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

 Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema Wizara itaendelea kuhakikisha miradi ya Viwanja vya Ndege nchini inaendelea kutekelezwa ili kuongeza huduma ya usafiri wa Anga na hivyo kufungua na kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini.

 Amesema Serikali katika kuhakikisha inaendelea kuimarisha shughuli utalii, biashara na kilimo,Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania inaendelea na hatua za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ya viwanja vipya vya Serengeti, Kagera na Njombe na mara baada ya kukamilika itatafuta fedha kwaajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

 Awali akitoa taarifa ya mradi wa Jengo la Viongozi Mashuhuri, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Abdul Mombokaleo amesema mradi huo ni sehemu ya utakelezaji wa mpango mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kuhusu uimarishaji wa Miundombinu na huduma za Viwanja vya Ndege.

 Jengo la Viongozi Mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, limejengwa mahsusi kwaajili ya kuhudumia wageni na Viongozi mashuhuri wa ndani na nje ya nchi. Jengo hilo ni hatua muhimu katika kuimarisha taswira ya Taifa na kuongeza hadhi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere katika ngazi ya kimataifa.


















 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...