-Rasimu ya Waraka wa Mapendekezo ya Baraza la Mawaziri ipo Tayari : Dkt. Kiruswa

Na Wizara ya Madini, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Madini inaendelea na mchakato wa kuanzisha Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Jiosayansi Tanzania (Tanzania Geoscientists Registration Board – TGRB), ambapo kwa sasa ipo katika hatua ya kukusanya maoni na mapendekezo ya wadau kabla ya kuanzishwa rasmi kwa bodi hiyo.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema hayo leo Januari 28, 2026, Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukene, Mhe. Stephano Luhende, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kuanzisha bodi hiyo ili kuongeza ufanisi katika sekta ya madini nchini.

Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa baadhi ya taratibu tayari zimekwisha tekelezwa, ikiwemo uandaaji wa rasimu ya Waraka wa Mapendekezo ya Baraza la Mawaziri kuhusu kuanzishwa kwa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Jiosayansi Tanzania.

Amefafanua kuwa kwa sasa Wizara ya Madini inaendelea na zoezi la kukusanya na kuchambua maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu masuala yatakayowezesha bodi hiyo kuanzishwa na kujiendesha kwa ufanisi, ikiwemo masuala ya uendeshaji na vyanzo vya fedha.

Ameongeza kuwa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la ukusanyaji na uchambuzi wa maoni, Wizara itawasilisha waraka huo katika ngazi za maamuzi za Serikali, ambazo ni kikao cha kitaalamu cha Makatibu Wakuu na kikao cha Baraza la Mawaziri, kwa ajili ya kujadiliwa na kupata ridhaa ya kuanzishwa rasmi kwa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Jiosayansi Tanzania.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...