Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro imepokea tuzo ya uongozi bora wa kukuza na kuwezesha mazingira bora ya Biashara, baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika tathmini ya mazingira ya biashara iliyofanyika mkoani humo.

Tuzo hiyo, inayojulikana kama Kilimanjaro Award for Pro-Business Environment, imetolewa wakati wa kikao cha Baraza la Biashara la mkoa wa Kilimanjaro lililofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Moshi, kilichowakutanisha viongozi wa serikali, wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali wa sekta binafsi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema kuwa serikali itaendelea kuweka na kuboresha mazingira rafiki ya biashara ili kuwawezesha wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa uhuru na ufanisi, kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

Babu alisisitiza kuwa mamlaka za ukusanyaji wa mapato, ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na halmashauri, hazipaswi kufunga biashara za wafanyabiashara pale wanapokuwa na madeni, bali zinapaswa kufanya mazungumzo na kufikia makubaliano ya namna bora ya ulipaji wa madeni hayo.

Alieleza kuwa hatua hiyo itawawezesha wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao huku wakitekeleza wajibu wao wa kulipa madeni kwa utaratibu uliokubaliwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, ameishukuru serikali ya mkoa kwa kutambua juhudi zinazofanywa na wilaya hiyo katika kuboresha mazingira ya biashara.

Amesema kuwa tuzo hiyo ni chachu ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kudumisha na kuimarisha mazingira rafiki kwa wafanyabiashara.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...