NA DIANA BYERA_BUKOBA.

Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera, Hamimu Mahmoud, ametoa wito kwa wanachama wote wa chama hicho, viongozi pamoja na waliogombea nafasi mbalimbali kukubaliana na matokeo ya uchaguzi na kutoa ushirikiano kwa viongozi waliochaguliwa.

Amesema kuwa uchaguzi tayari umekamilika na sasa ni wakati wa kuwaacha viongozi waliochaguliwa kufanya kazi ya kutekeleza Ilani ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2025 hadi 2030.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 49 ya Chama Cha Mapinduzi yaliyofanyika katika viwanja vya Mikoni, Hamimu alisema kuwa ushirikiano na mshikamano wa wanachama wote ni msingi wa kuhakikisha Ilani ya chama inatekelezwa kwa ufanisi wa asilimia 100.

Alieleza kuwa chama kinaendelea kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wanachama ambao hawakufanikiwa kupata nafasi za uongozi lakini wanaendelea kufanya vitendo vya kuhujumu kazi zinazotekelezwa na viongozi waliochaguliwa.

Alisisitiza kuwa siasa za kugombea zina muda wake na kwamba kwa sasa ni wakati wa kufanya kazi, aliongeza kuwa ndani ya CCM watu hutambuliwa kwa matendo yao, na kwamba chama hakitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka maamuzi ya wengi.

Alisisitiza kuwa makundi yameisha na sasa ni muda wa viongozi waliochaguliwa kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Hamimu pia aliwahimiza viongozi waliochaguliwa katika ngazi za udiwani na ubunge kuhakikisha sherehe za mwaka huu zinatumika kama fursa ya kuwashukuru wananchi kwa imani waliyoendelea kukionyesha Chama Cha Mapinduzi kwa kuwatumikia kwa dhati katika sekta muhimu ikiwemo afya, elimu, miundombinu na barabara.

Aidha, aliwaomba wananchi wa vijijini kuendelea kutumia nishati safi ili kupunguza uharibifu wa mazingira, kuendelea kupanda miti kwa wingi, kutumia majiko banifu pamoja na kupunguza uvunaji wa misitu ili kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira.

Kwa niaba ya madiwani wa Bukoba Vijijini, Ashrafu Nyangasha alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi ndicho chama chenye dira ya kuleta maendeleo kwa kila mwananchi na kuboresha maisha ya Watanzania kwa ujumla.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...