Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Januari 21, 2026 wakati wa kuzikumbusha taasisi binafsi na za umma zinazochakata taarifa binafsi kujisajili Katika tume ya Ulinzi wa Taarifa binafsi (PDPC).

Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
TUME  ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imetoa tahadhari kwa taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi kwamba hatua kali za kisheria zitaanza kuchukuliwa mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha miezi mitatu ya nyongeza ya kujisajili.

Tahadhari hiyo inafuatia uamuzi wa Serikali wa kutoa muda wa nyongeza kuanzia Januari 8, 2026 hadi Aprili 8, 2026, kwa taasisi ambazo bado hazijazingatia matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44, kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Januari 22, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, amesema kipindi hicho ni cha mwisho cha hiari kabla ya kuanza utekelezaji mkali wa Sheria kwa taasisi zitakazokaidi.

Ameeleza kuwa baada ya Aprili 8, 2026, PDPC itaanza mara moja kufanya ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria kwa taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya, kuhifadhi, kuchakata au kusafirisha taarifa binafsi ndani na nje ya nchi.

Dkt. Mkilia amesema ukaguzi huo utalenga kubaini taasisi zitakazobainika kuendesha shughuli hizo bila usajili au kinyume na masharti ya Sheria na Kanuni zake, hatua itakayofungua mlango wa kuchukuliwa kwa hatua za kisheria.

Kwa mujibu wa PDPC, adhabu kwa watakaokiuka Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni pamoja na kutozwa faini, kifungo au adhabu zote kwa pamoja, sambamba na ulazima wa kulipa fidia kwa waathirika wa ukiukwaji wa haki ya faragha.

Tume imefafanua kuwa kuvunja faragha au kutumia taarifa binafsi bila ridhaa ya mhusika ni kosa linalomuwajibisha mhusika binafsi bila kujali hadhi, ukubwa au aina ya taasisi husika.

Katika wito wake, PDPC imezitaka taasisi zote za umma na binafsi kutumia ipasavyo kipindi cha miezi mitatu kilichotolewa ili kujisajili, kuimarisha mifumo ya ulinzi wa taarifa binafsi na kuepuka hatua za kisheria zitakazoanza kuchukuliwa mara baada ya muda huo kumalizika.

Sambamba na hilo, PDPC imetangaza kushiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa mwaka 2026 kuanzia Januari 26 hadi 30, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa umma kuhusu haki ya faragha na wajibu wa taasisi katika kulinda taarifa binafsi.

PDPC imesisitiza itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu na weledi kwa lengo la kulinda taarifa binafsi za Watanzania na kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia na huduma za kidijitali nchini.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...