Farida Mangube, Morogoro

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amewaondoa wasiwasi wanafunzi wanaosoma sayansi ya wanyama, viumbe maji na nyanda za malisho kwa kuwahakikishia kuwa hawatapoteza chochote kutokana na masomo yao, kwani sekta ya Mifugo na Uvuvi ina fursa nyingi za ajira na biashara.

Balozi Dkt. Bashiru ametoa kauli hiyo alipokutana na wanafunzi wa shahada ya kwanza wa nyanda za malisho waliokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo ya upandaji wa malisho ya mifugo katika shamba darasa la Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), wakati wa ziara yake ya siku moja chuoni hapo.

Katika ziara hiyo, Waziri pia alipata fursa ya kuzungumza na wataalamu wa SUA pamoja na wakurugenzi wa taasisi za Mifugo na Uvuvi zilizo chini ya Wizara yake.

Amesema kuwa bila uwepo wa malisho bora haiwezekani kufuga kwa tija, hasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayolazimisha kuwekwa mkazo mkubwa kwenye uzalishaji wa malisho.

Alieleza kuwa nyasi za asili katika nyanda za malisho zimeanza kupoteza sifa kutokana na ukame wa muda mrefu, hali iliyosababisha wafugaji wengi kupoteza mifugo yao.

“Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine ni miongoni mwa vyuo vyenye heshima kubwa nchini katika mafunzo, ushauri wa kitaalamu na utafiti kwenye kilimo, mifugo, uvuvi na misitu.” alisema Waziri.

Ameongeza kuwa Wizara yake imepewa maelekezo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo inaelekeza kuachana na ufugaji wa kienyeji na kuelekea ufugaji wa kisasa wenye tija na ufanisi.

Aliwahimiza wanafunzi kutumia vyema elimu wanayoipata kwa kufanya tafiti zitakazowasaidia kuingia sokoni na kujiajiri, akisisitiza kuwa sekta ya malisho ni biashara kubwa na wale waliothubutu wameanza kufanikiwa.

“Msidhani mnapoteza muda. Eneo la malisho sasa ni biashara kubwa. Kuna biashara ya mbegu za malisho, uzalishaji wa malisho yenyewe na usindikaji wake ili kuyaongezea thamani. Nawapongezeni kwa kuchagua kusoma fani hii muhimu,” alisema.

Waziri alisema Wizara imekubaliana na uongozi wa SUA kuunda kamati ya pamoja itakayojumuisha Wizara na Chuo hicho, itakayosimamiwa na ofisi yake kwa kushirikiana na SUA, kwa lengo la kuimarisha tafiti, mafunzo na ushauri wa kitaalamu, hususan katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, mabwawa, uzalishaji wa malisho na matumizi ya maabara.

“Nimetembelea maabara na nimejionea kuwa ni za kisasa na zina viwango vya kimataifa,” aliongeza.

Akizungumza na watendaji wa Wizara pamoja na menejimenti ya SUA, Dkt. Bashiru alisema bado kuna ufa mkubwa wa kimahusiano na kiutendaji kati ya Wizara na taasisi zake, na kusisitiza kuwa njia pekee ya kuuziba ni kupitia ushirikiano wa karibu.

Alisema mchango wa sekta ya Mifugo na Uvuvi katika uchumi wa taifa bado hauridhishi ikilinganishwa na rasilimali zilizopo. Alibainisha kuwa sekta ya mifugo ina mchango mzuri, lakini sekta ya uvuvi bado ina mchango mdogo licha ya Tanzania kuwa na rasilimali nyingi za uvuvi ukilinganisha na nchi nyingi za Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA, Profesa Raphael Chibunda, alisema kuwa licha ya changamoto ya bajeti, chuo kimekuwa kikitenga shilingi bilioni 1 kila mwaka kwa ajili ya utafiti, hususani kujenga uwezo wa watafiti wapya, kutokana na ushindani mkubwa wa kupata fedha za tafiti.

Alisema mpango huo umezaa matunda na kuiomba Wizara pamoja na taasisi zake kuweka utaratibu wa kutenga fedha mahsusi kwa ajili ya kuendeleza utafiti, hususan kwa watafiti chipukizi.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...