Na Pamela Mollel Arusha

Serikali imezitaka taasisi za umma na binafsi nchini kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa wananchi na watumishi wake, ili kuimarisha faragha, usalama wa taarifa na haki za msingi za wananchi katika mazingira ya uchumi wa kidijitali.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Anjellah Kairuki, wakati wa hafla ya kufunga mafunzo maalum kwa Maafisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi yaliyofanyika jijini Arusha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Kairuki alisema kuwa utoaji wa elimu kwa umma ni nguzo muhimu ya utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, akibainisha kuwa uelewa mdogo wa sheria hiyo unaweza kusababisha ukiukwaji wa faragha na haki za wananchi.

“Maafisa wa ulinzi wa taarifa binafsi mliohitimu leo mna wajibu wa kisheria kuhakikisha elimu ya ulinzi wa taarifa binafsi inatolewa ndani ya taasisi zenu. Serikali haitakubali visingizio vya kutokujua sheria, uzembe au ucheleweshaji wa utekelezaji,” alisema Waziri Kairuki.

Waziri huyo alisisitiza kuwa elimu hiyo inapaswa kutekelezwa kitaifa kwa kushirikiana na taasisi za umma na binafsi pamoja na sekta mbalimbali ikiwemo fedha, mawasiliano, afya, elimu, vyombo vya habari, asasi za kiraia na makundi mengine yote yanayohusika na ukusanyaji au uchakataji wa taarifa binafsi.

Aidha, alieleza kuwa kila Afisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi ana wajibu wa kuhakikisha taasisi yake inazingatia kikamilifu kanuni za uhalali, uwazi, matumizi ya taarifa kwa madhumuni mahususi, usalama wa taarifa na heshima ya faragha ya wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Bw. Adadi Mohamed, alisema kuwa Tume itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kufahamu wajibu na haki zao, akibainisha kuwa uchumi wa kidijitali una uhusiano wa moja kwa moja na sekta ya utalii.

Bw. Adadi alionya kuwa kutotekeleza Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni sawa na kuweka rehani faragha, usalama na haki za msingi za wananchi wanaohudumiwa na taasisi za umma na binafsi.

“Kukosekana kwa ulinzi wa taarifa binafsi kunahatarisha imani ya wananchi na kudhoofisha maendeleo ya uchumi wa kidijitali,” alisema.

Akielezea lengo la mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia, alisema kuwa mafunzo hayo yalilenga kuwaandaa Maafisa wa rasilimali watu na Maafisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi wenye uwezo wa kusimamia utekelezaji wa sheria ndani ya taasisi za umma na binafsi.

Dkt. Mkilia alifafanua kuwa kusudio kuu ni kuhakikisha ukusanyaji, uchakataji, uhifadhi na matumizi ya taarifa binafsi vinafanyika kwa kuzingatia kikamilifu matakwa ya Sheria, kanuni na viwango vya kitaaluma vinavyolinda haki ya faragha ya wananchi kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Kwa mujibu wa Tume hiyo, jumla ya taasisi 178 zilishiriki mafunzo hayo, ambapo taasisi 28 zilitoka serikalini, taasisi 38 kutoka sekta ya utalii na taasisi 112 kutoka sekta nyingine mbalimbali zinazojihusisha na ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...