Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji uwekezaji wa ndani kwa mwaka 2026. Uzinduzi huo umefanyika leo Januari 16, 2026 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) Gilead Teri, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji uwekezaji wa ndani kwa mwaka 2026. Uzinduzi huo umefanyika leo Januari 16, 2026 jijini Dar es Salaam.


SERIKALI imewataka Watanzania kutumia ardhi wanayomiliki kama mtaji wa kuingia kwenye uwekezaji, badala ya kuiacha bila kuendelezwa, hatua itakayosaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa leo Januari 16, 2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji uwekezaji wa ndani kwa mwaka 2026.

Profesa Kitila amesema moja ya maeneo muhimu yatakayofanyiwa kazi kupitia kampeni hiyo ni suala la ardhi, akieleza kuwa Watanzania wengi wanamiliki maeneo makubwa ya ardhi lakini hawana uelewa wa namna ya kuyatumia kiuchumi.

Amesema kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), wananchi watapatiwa elimu juu ya namna ya kuyakabidhi maeneo yao kwa mamlaka hiyo ili kusaidiwa kupata wawekezaji watakaowekeza katika ardhi hizo kwa mfumo wa ubia au makubaliano rasmi.

“Lengo ni kuwasaidia Watanzania kubadilisha ardhi yao kuwa mali yenye thamani, inayoweza kuleta ajira, mapato na maendeleo endelevu,” amesema Profesa Kitila.

Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwahamasisha Watanzania kutumia rasilimali walizonazo, ikiwemo ardhi, kama nyenzo ya kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi sambamba na uwekezaji wa wageni.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Masoko kutoka Benki ya Equity, Shumbana Walwa amesema ufadhili na ushirikiano kati ya benki hiyo na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) utaleta manufaa makubwa kwa Watanzania, hususan katika kuwawezesha wawekezaji wa ndani kupata mitaji na huduma za kifedha kwa urahisi.

Amesema kupitia ushirikiano huo, Benki ya Equity itaendelea kutoa elimu ya kifedha, ushauri na bidhaa mbalimbali za kifedha zitakazowawezesha Watanzania kubadilisha mawazo yao ya kibiashara kuwa miradi halisi ya uwekezaji.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji wa ndani, kukuza biashara ndogo za kati na Kubwa pamoja na kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, amesema mamlaka hiyo imejipanga kuzunguka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kushirikiana na Benki ya Equity, kwa lengo la kutoa elimu ya uwekezaji na kuwaunganisha wamiliki wa ardhi na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Teri amesema kwa mwaka 2026, TISEZA inalenga kusajili miradi 1,500 ya uwekezaji, ambapo sehemu kubwa inalenga kuwahusisha Watanzania moja kwa moja kupitia umiliki wa ardhi na miradi ya ubia.

Amebainisha kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mageuzi makubwa ya sekta ya uwekezaji chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kuwawezesha Watanzania kiuchumi na kuongeza ushiriki wao katika uwekezaji.

Kwa upande wake, mwekezaji wa ndani, Willium Ngeleja, amesema uzinduzi wa kampeni hiyo utakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania, kwani utaongeza uelewa juu ya fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuwahamasisha wananchi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi.

Ngeleja amesema kampeni hiyo itasaidia kubadilisha mtazamo wa Watanzania kuhusu uwekezaji, hasa kwa kuwa itatoa elimu ya kina kuhusu taratibu, vivutio na namna ya kuanza kuwekeza hata kwa mtaji mdogo.

Ameongeza kuwa jitihada za serikali katika kuhamasisha uwekezaji wa ndani zitachochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha ushiriki wa wazawa katika miradi mikubwa ya maendeleo nchini.






Matukio mbalimbali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...