FARIDA MANGUBE,Morogoro
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Tanzania ina mifumo imara ya kusimamia rasilimali na kudhibiti rushwa, hali inayofanya nchi iendelee kuwa kielelezo na mwalimu kwa mataifa mengi ya Afrika katika masuala ya utawala bora.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo Januari 26, 2026, mkoani Morogoro, alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu ameipongeza TAKUKURU kwa kazi kubwa wanayoifanya ambayo imeongeza uaminifu wa Tanzania ndani na nje ya nchi.
Amesema mifumo ya udhibiti iliyojengwa imeifanya Tanzania isimame imara hata mbele ya changamoto za kiutawala zinazozikumba nchi nyingine.
“Wapo watu na hata mataifa yanayoikosoa Tanzania mitandaoni, lakini ukweli ni kwamba wengi wao wanahangaika kwa sababu wameshindwa kufikia kiwango cha mifumo ya udhibiti tuliyonayo hapa nchini,” amesema Dkt. Mwigulu.
Katika kuwasilisha ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan, Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa Rais hapendi wala havumilii rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, au uzembe kazini, na kwamba dhamira yake ya kulinda utu wa mwananchi na kuleta maendeleo ya kweli inategemea sana uadilifu wa taasisi za udhibiti.
Amebainisha kuwa Rais Samia ameendelea kuchukua hatua za makusudi kuziimarisha taasisi hizo kwa kuziongezea rasilimali watu, bajeti, miundombinu, pamoja na kufanya marekebisho ya kisheria ili kuzipa mamlaka na “meno” ya kutosha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa kupitia kazi nzuri inayofanywa na TAKUKURU, rasilimali za taifa zitatumika ipasavyo kwa manufaa ya Watanzania na kuleta maendeleo ya kweli na endelevu.
Amewahakikishia viongozi wa TAKUKURU kuwa wanayo dhamana na uungaji mkono wa asilimia 100 kutoka ngazi ya juu ya uongozi wa nchi, huku akiwataka waendelee kupambana na vitendo vyote vinavyoharibu misingi ya utawala bora.
Akieleza mafanikio ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, TAKUKURU imefanikiwa kuokoa fedha hizo kupitia operesheni za uchunguzi, fedha ambazo zimerejeshwa Serikalini na nyingine kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama ilivyokusudiwa.
Katika kipindi hicho pia TAKUKURU ilifuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 619 yenye thamani ya Shilingi bilioni 553.45, na kufanikiwa kuokoa Shilingi milioni 173.5 zilizokuwa hatarini kupotea kwa njia za rushwa.
Kwa upande wa mapambano ya kisheria, TAKUKURU iliendesha kesi 489 mahakamani, ambapo Jamhuri ilishinda kwa asilimia 68.8 ya kesi zilizotolewa uamuzi, kiwango ambacho kinatarajiwa kuongezeka ifikapo Juni 2026.
Vilevile, TAKUKURU ilishiriki katika uangalizi wa chaguzi katika nchi za Mauritius, Botswana na Msumbiji, hatua iliyolenga kudhibiti vitendo vya rushwa katika michakato ya uchaguzi.
Katika kuimarisha uhusiano na wananchi, TAKUKURU imeendelea kutekeleza Programu ya TAKUKURU Rafiki, inayolenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika utoaji wa huduma za umma kabla hazijazaa mianya ya rushwa. Programu hiyo imeelezwa kuonyesha mafanikio makubwa kwa mujibu wa mrejesho wa wananchi.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...