Na OWM- TAMISEMI, Dodoma

Tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka wa fedha 2024/25 imeonesha mafanikio makubwa, ambapo rangi ya kijani imetawala katika viashiria vingi vya utekelezaji, ikiwa ni ishara ya kufanya vizuri kwa mikoa na halmashauri nchini.

Hayo yamesemwa leo Januari 22,2026 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, wakati akifungua mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Prof. Shemdoe amesema Taifa limeendelea kupiga hatua kubwa katika kuboresha hali ya lishe kwa wananchi, hali inayochangia kuimarisha nguvu kazi yenye afya bora na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

“Nawashukuru Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Maafisa Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa pamoja na viongozi na watendaji wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri kwa kazi kubwa ya kusimamia, kuratibu na kutekeleza Mkataba wa Lishe,” amesema Prof. Shemdoe.

Amewahakikishia kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI itaendelea kushirikiana na kuwapa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kupunguza na hatimaye kutokomeza kabisa matatizo ya lishe nchini inafikiwa.

Amebainisha  kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa usia wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyehimiza kuimarishwa kwa sekta za Elimu, Afya na Uchumi ili kupambana na maadui watatu wa Taifa ambao ni ujinga, maradhi na umasikini.

Prof. Shemdoe amesema uwekezaji katika lishe ni mkakati wa kiuchumi wenye tija kubwa, na kwamba Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imeipa kipaumbele kujenga jamii yenye afya kwa kuzingatia lishe bora ili kila mwananchi astawi.

Aidha, amesema Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025/30, ibara ya 2.3.2 (xi), imetambua umuhimu wa lishe katika kulinda na kujenga afya za wananchi, ambapo CCM itaendelea kuhimiza na kusimamia upatikanaji wa lishe bora kwa wote.

Akizungumza kuhusu dhana ya lishe bora, Prof. Shemdoe amesema ni matokeo ya kutokuwepo kwa magonjwa mwilini pamoja na ulaji sahihi wa vyakula vyenye virutubishi vyote vinavyohitajika.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuanza utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, hatua itakayosaidia kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma stahiki za afya na kushinda adui maradhi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amesema lishe ni suala la msingi katika ukuaji wa binadamu kiakili na kimwili, sambamba na kuongeza tija katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Naye,Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu  anayeshughulikia afya Prof.Tumaini Nagu amesema serikali itaendelea  kusimamia kwa karibu utoaji wa huduma za lishe katika Mikoa na Halmashauri zote nchini.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...