Na Mwandishi wetu, Dodoma.


Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Ashatu Kijaji (Mb) wiki hii ameendelea kuongoza menejimenti ya wizara hiyo mbele ya kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuelezea kazi,majukumu ,muundo na changamoto za wizara hiyo na taasisi zake.

Katika mawasilisho mbalimbali yaliyofanyika mbele ya kamati hiyo kutoka kwa taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ikiongozwa na Kamishna wa uhifadhi Bw. Abdulrazaq Badru iliwasilisha taarifa yake ikiwa na mafanikio makubwa katika uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.

Katika kikao hicho Ngorongoro iliwakumbusha waheshimiwa wabunge kuhusiana na historia isiyofutika ya faru wakubwa wawili ambao waliishi katika hifadhi hiyo kwa mda mrefu zaidi. Faru hao ni Fausta aliyezaliwa mwaka 1965 na kufa mwaka 2019 na faru John aliyezaliwa mwaka 1978 na kufa mwaka 2016.

Ngorongoro imewaweka kwenye historia faru hao ili kuwaonesha watanzania umuhimu wa kuhifadhi faru ambapo idadi yake ndani ya hifadhi hiyo inazidi kuongezeka na kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika uingizaji wa fedha za kigeni.

Faru John ndani ya hifadhi ya Ngorongoro alijulikana pia kama Bingwa wa mapenzi ama dume la mbegu kutokana na kuweza kuizunguka hifadhi yote akitafuta faru majike ili aweze kushiriki nao tendo la ndoa huku upendo wake ukitawaliwa na wivu wa kupindukia.

Tabia nyingine ya faru huyo ilikuwa ni utawala wa muda mrefu ndani ya hifadhi hivyo alikuwa chanzo kikubwa cha migogoro na kutaka kila faru jike awe naye peke yake hali ambayo mwaka 2011 alimuua faru CHAUSI kwa kugombea jike hii inadhihirisha ni jinsi gani mapenzi yanaua.

Tofauti na faru John, Faru Fausta, ndiye faru pekee aliyeweza kuishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwa muda mrefu wa miaka 54 na inasemekana pia amevunja rekodi ya kidunia kuwa miongoni mwa faru wachache weusi walioweza kuishi miaka mingi.

Faru Fausta licha ya kupandwa na madume mbalimbali ikiwenmo faru John, hakubahatika kupata mtoto na kwa mujibu wa wataalam wa wanyama haikubainika ni kwanini faru Fausta katika umri wake wote wa miaka 54 hakujaaliwa uzazi.

Kisayansi faru anaweza asipate mtoto kutokana na kuwa na matatizo katika mfumo wa uzazi ikiwa ni pamoja na kuchelewa kupata mimba ambapo faru akiwa na hali hiyo katika umri unaotakiwa anakuwa na homoni kiasi kidogo za jike na hivyo kushindwa kupata mimba.

Wataalam wanasema kuwa Faru Fausta inawezekana aliishi muda mrefu kwa sababu hakuwa na msongo wa mawazo wa kushika mimba,kulea watoto wala kunyonyesha zaidi ya kula bata na kushiriki mapenzi na faru wenzake.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...