Na Mwandishi Wetu
NAIBU Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Masoko na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Salehe Beleko, amewataka viongozi na makamanda wa vituo vya wakala huo kuimarisha nidhamu ya mipango, uwazi wa mapato na utoaji wa huduma kwa kuzingatia misingi ya “Kazi na Utu”.
Akizungumza leo Februari 19, 2026 katika siku ya pili ya Mkutano wa Nne wa Viongozi na Makamanda wa Vituo vya TFS unaoendelea katika Ukumbi wa Hoteli ya Cate, Morogoro, Beleko alisisitiza kuwa mafanikio ya uhifadhi yanategemea ubora wa mipango na utekelezaji wake.
“Tunapoandaa mpango mkakati na mpango wa kibiashara, tuzingatie rasilimali tulizonazo. Fedha ni haba lakini mahitaji ni mengi, hivyo lazima tuweke vipaumbele vitakavyotupeleka moja kwa moja katika kuimarisha uhifadhi,” alisema.
Alionya kuwa ongezeko la carry overs na reallocation ni dalili ya udhaifu katika upangaji wa bajeti na mtiririko wa fedha (cash flows), akitahadharisha kuwa taasisi isipopanga vizuri, hujiandalia mazingira ya kushindwa.
Kwa upande wa leseni na matumizi ya rasilimali, Beleko alieleza kuwa kumekuwapo na tofauti kati ya kiasi kilichopangwa kuvunwa na kile kinachovunwa katika baadhi ya maeneo, huku malengo ya mapato yakifikiwa kupitia mifumo isiyo sahihi.
“Hakikisheni huduma zinatolewa kwa wateja waliopitia taratibu zote za kisheria—kamati za uvunaji za wilaya, vyeti vya mgao na leseni halali. Tusikusanye mapato nje ya mfumo,” alisisitiza.
Aidha, alikemea matumizi holela ya mashine za kuchakatia na misumeno ya moto ndani ya hifadhi bila vibali maalum, akitaka taratibu zifuatwe kikamilifu ili kulinda rasilimali na mapato ya serikali.
Katika kuboresha uwajibikaji, alihimiza matumizi ya teknolojia za kisasa katika upimaji wa rasilimali za misitu ili kuzuia upotevu wa mapato na mianya ya udanganyifu.
Hata hivyo, pamoja na msisitizo wa nidhamu ya kifedha na kiutendaji, alirejea kaulimbiu ya “Kazi na Utu”, akitaka wahifadhi na watumishi wote kutoa huduma kwa heshima na kuwachukulia wateja kama wadau, si wahalifu.
“Tuwahudumie kwa heshima. Wapo wanaokengeuka, lakini tuna wajibu wa kuwabadilisha kuwa wateja wazuri. Huduma bora inaleta tabasamu kwa Watanzania,” alisema.
Mkutano huo unaendelea kujadili mikakati ya kuimarisha uhifadhi, kuongeza mapato halali na kuboresha usimamizi wa mashamba na hifadhi za misitu nchini.



.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...