Benki ya Exim Tanzania imehitimisha rasmi kampeni yake ya ‘Chanja Kijanja, Dili Ndio Hili’ kwa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi iliyofanyika katika tawi lake jipya la Ubungo. Kampeni hiyo, iliyodumu kwa miezi miwili, ililenga kuhamasisha matumizi ya kadi za benki katika malipo ya kila siku na kuendeleza utamaduni wa miamala ya kidijitali isiyotumia fedha taslimu.
Katika kilele cha hafla hiyo, Asif K. Dhalla alitangazwa na kukabidhiwa zawadi kuu ya kiasi cha shilingi milioni 15. Aliakber Zoeb Hakimjee alipokea shilingi milioni 10 kama mshindi wa pili, huku John Estomih Kweka akijishindia shilingi milioni 5 kama mshindi wa tatu. Mbali na zawadi hizo kuu, washindi zaidi ya 60 wa kila wiki na mwezi walijishindia Zawadi zao; washindi wa kila wiki walizawadiwa shilingi 100,000 kila mmoja na washindinwa kila mwezi walipokea shilingi 200,000 kila mmoja, ikiwa ni motisha kwa matumizi endelevu ya kadi katika kipindi chote cha kampeni.Kupitia kampeni hiyo, wateja pia walipata fursa ya kunufaika na ofa maalum, punguzo la bei na zawadi mbalimbali walipotumia kadi zao katika maeneo washirika kama Shoppers Plaza, Village Supermarket, Karambezi Café pamoja na CIP Lounge ya uwanja wa ndege.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Stanley Kafu, alisema kampeni hiyo imekuwa njia ya kuonesha kuthamini wateja wa benki hiyo na kuimarisha uelewa wa faida za malipo ya kidijitali. Alisisitiza kuwa matumizi ya kadi si tu rahisi na salama, bali pia yanaweza kuwa na manufaa kwa mteja.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala na Mabadiliko ya Kidijitali wa Benki ya Exim Silas Matoi, alieleza kuwa mwitikio wa wateja umeonesha mabadiliko chanya katika namna wanavyoipokea teknolojia ya fedha. Alibainisha kuwa ongezeko la matumizi ya kadi ni ishara ya safari inayoendelea kuelekea uchumi usiotegemea fedha taslimu.
Makabidhiano hayo yalifanyika chini ya usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania ili kuhakikisha mchakato wote unafuata taratibu na kanuni zilizowekwa. Mwakilishi wa Bodi hiyo, Neema Tatock, alithibitisha kuwa droo zote ziliendeshwa kwa uwazi na haki, na kutoa uhakika kwa washiriki wote.
Akizungumza kwa furaha baada ya kupokea zawadi yake, mshindi wa zawadi kuu Asif K. Dhalla alisema ushindi huo umempa furaha, alieleza kuwa kampeni hiyo imempa motisha zaidi ya kuendelea kutumia kadi katika miamala yake ya kila siku.
Exim Bank imetoa shukrani kwa wateja wake wote kwa ushiriki wao mkubwa pamoja na washirika wake ikiwemo, Shoppers Plaza, Village Supermarket, Karambezi Café na CIP Lounge, kwa mchango wao katika kufanikisha kampeni hiyo.
Benki hiyo imeeleza kuwa itaendelea kubuni na kuboresha huduma za kidijitali zinazomrahisishia mteja kufanya miamala kwa usalama na ufanisi, sambamba na kuunga mkono juhudi za taifa katika kukuza mfumo wa malipo wa kisasa na jumuishi.

.jpeg)

.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...