Benki ya Stanbic kwa kushirikiana na Uwezo Tanzania wamezindua mpango madhubuti wa maktaba za shule unaoanza katika shule za msingi 45 zilizopo Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe, kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa vitabu na vifaa vya kujifunzia vinavyolingana na mtaala mpya wa taifa.

Mpango huu unalenga uanzishwaji wa maktaba hizo pamoja na kutoa vitabu vya hadithi na rasilimali za kielimu zilizobuniwa ili kuimarisha elimu msingi, kukuza ujuzi wa kusoma na kuandika, pamoja na kuongeza ushiriki wa wanafunzi katika madarasa na jamii kwa ujumla.

Kupitia Mpango wa My Village, UWEZO inaunga mkono maktaba za jamii kwa kuimarisha elimu msingi kwa watoto kwa kutoa vitabu vinavyoendana na mtaala wa taifa. Tukio hili la kukabidhi vitabu linaendana na Mpango wa Kitaifa wa Maendeleo ya Elimu wa KKK uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 29 Januari. Kwa kuboresha upatikanaji wa vitabu na vifaa vya kujifunzia. mpango huu unachangia kuboresha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, pamoja na kuwezesha ufuatiliaji na uungaji mkono wa elimu msingi kwa watoto katika ngazi ya jamii.

Mpango huu unafadhiliwa na Benki ya Stanbic Tanzania. Fedha kutoka Benki ya Stanbic Tanzania zitasaidia ununuzi wa vitabu vinavyoendana na mtaala pamoja na vitabu vya ziada, ambapo inatarajiwa kufaidisha takribani watoto 33,619 kila mwaka kwa kipindi cha miaka 10 hadi 20.

“Ushirikiano huu unaakisi namna Benki ya Stanbic inavyotekeleza uwekezaji wake wa kijamii, kwa kuzingatia miradi yenye manufaa ya moja kwa moja na inayoweza kupimwa matokeo yake. Kama ilivyo kwa programu zetu zilizopita katika sekta ya elimu na maendeleo ya jamii, mpango huu unatuwezesha kukidhi mahitaji halisi ya jamii zetu, na inaendana na kauli mbiu yetu kuwa Tanzania ni nyumbani, na tunachochea ukuaji wake,” amesema Dickson Senzi, Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano, Benki ya Stanbic Tanzania.

Pamoja na Benki ya Stanbic Tanzania, Uwezo Tanzania pia inafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), Maktaba ya Taifa ya Tanzania, na wachapishaji wa vitabu wa Mkuki na Nyota. Aidha, uanzishwaji wa maktaba za shule unatarajiwa kuwahamasisha walimu na timu za usimamizi wa shule kushiriki kikamilifu katika juhudi za elimu ngazi ya kijiji kwa kutoa maeneo na miundombinu ya maktaba ndani ya shule. Njia hii itawezesha watoto na wazazi kutembelea maktaba pamoja, na kusaidia usomaji wa vitabu vya mtaala na vile vya ziada shuleni na nyumbani.

Zaidi ya hayo, walimu wanaoshiriki katika mpango huu watapatiwa vijitabu vyenye maudhui ya kujifunzia kusoma, kuandika na kuhesabu, na mahudhurio ya maktaba yatarekodiwa kwa utaratibu maalum. Walimu pia watahamasishwa kuchangia vitabu vingine vinavyopatikana shuleni mwao na kuviongeza katika maktaba za shule.

Mpango huu ni hatua muhimu katika kuboresha matokeo ya elimu msingi, kukuza utamaduni wa kusoma, na kuendeleza ubunifu na fikra pevu miongoni mwa wanafunzi. Kupitia mpango huu, Uwezo Tanzania inathibitisha dhamira yake ya kuhakikisha upatikanaji wa haki wa rasilimali bora za elimu na kuwawezesha wanafunzi kote Tanzania.

Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano, Benki ya Stanbic Tanzania, Dickson Senzi (kulia), na Mkurugenzi Mtendaji wa Uwezo Tanzania, Baraka Mgohamwende (kushoto), wakimkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Sunday Deogratius, vitabu vilivyofadhiliwa na Benki ya Stanbic kwa ajili ya kuanzisha maktaba 45 katika shule za msingi za Wilaya ya Ludewa. Hafla hiyo fupi ilifanyika jijini Dar es Salaam, jana.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...