Na Karama Kenyunko Michuzi Tv 

NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Amir, amewataka vijana kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa kupitia Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu ili waweze kutimiza ndoto zao na kujikwamua kiuchumi.

Aidha, amesikitishwa na idadi ndogo ya wabunifu waliojitokeza kuomba mkopo huo, huku akiitaka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Benki ya CRDB, wanaosimamia utekelezaji wa mfuko huo, kuendelea kutoa elimu kwa vijana ili wengi zaidi wanufaike.

Wanu ameyasema hayo leo, Februari 13, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha ya siku moja ya kuwajengea uwezo wabunifu na kuwatambua wanufaika wa mfuko huo. Amewahimiza vijana kutuma maombi kwa kuwa fedha zipo na hazijatumika ipasavyo.

Amesema katika kipindi cha miezi kumi, vijana saba pekee ndio walionufaika na mkopo wa jumla ya Sh milioni 767 kati ya Sh bilioni 4.6 zilizotengwa kwa ajili ya mfuko huo.

“Kwa idadi kubwa ya wabunifu tulionao nchini, matarajio yangu yalikuwa fedha hizi zingeshachukuliwa ndani ya mwaka mmoja. Nimeambiwa baadhi walikwama kutokana na kukosa taarifa sahihi au kutokukidhi vigezo vya kibiashara,” amesema Wanu.

Kutokana na changamoto hizo, ameagiza zifanyiwe kazi kwa kuandaliwa mafunzo maalum yatakayowawezesha wabunifu kupata uelewa na uwezo wa kukidhi masharti ya mkopo.

“Nitoe wito kwa COSTECH na CRDB kuendelea kuwapa elimu wabunifu. Kama kuna changamoto za kimfumo, zipatiwe ufumbuzi wa haraka ili fedha hizi ziwanufaishe walengwa kama ilivyokusudiwa,” amesisitiza.

Akinukuu taarifa ya Mkurugenzi wa CRDB, Wanu amesema vijana wenye uhitaji ni wengi, hivyo ni muhimu kubaini vikwazo vinavyowafanya wasifikie fursa hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa fedha zilizotolewa hazijafikia hata asilimia 10 ya kiasi kilichopo.

Amewahimiza vijana wenye ubunifu wa bidhaa au utoaji huduma kuendelea kuwasilisha maombi kupitia COSTECH na wasikate tamaa hata kama fomu zina maswali mengi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema mfuko huo wenye thamani ya Sh bilioni 4.6 hadi sasa umepokea maombi 100. 

Kati ya hayo, maombi 22 yamekamilika, 15 hayakukidhi vigezo vya kibiashara, na saba ndiyo yalikidhi vigezo. Wabunifu watatu tayari wamepokea fedha zao huku wanne wakiwa katika hatua za mwisho za kupatiwa mikopo.

Dkt. Nungu amesema lengo la mfuko huo ni kuwawezesha vijana wabunifu kupata mitaji, kukuza biashara zao na kurejesha mikopo ili fedha ziendelee kuwanufaisha wengine.

Mmoja wa wanufaika, Poul Musiba, ambaye kampuni yake inajihusisha na ufugaji wa nyuki, ameishukuru serikali kwa fursa hiyo. Amesema alipata mkopo wa Sh milioni 135 kati ya Sh milioni 200 alizoomba, hatua iliyomsaidia kupanua shughuli zake za uzalishaji.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...