*📌 Wateja wa awali zaidi ya elfu 20 kuunganishwa na huduma ya umeme katika Vitongoji vya mkoa huo. *
Morogoro📍
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, tarehe 6 Februari, 2026 amewapokea wakandarasi wawili kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA); watakaotekeleza Mradi mkubwa wa kusambaza umeme katika vitongoji 570 vya mkoa huo; ikielezwa kuwa Mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 91.
Wakandarasi hao ni kampuni ya Sagemcom Energy & Telecom SAS (Italia) na China Railway No. 4 Engineering Group Co. Ltd (China) ambao watasambaza umeme katika vitongoji 570 katika Mradi huo mkubwa kwa gharama ya shilingi bilioni 91.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwatambulisha wakandarasi hao, Mhe. Malima alisema Mradi huo ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma ya umeme wa uhakika hususan maeneo ya vijijini.
Mhe. Malima alisema kuwa Serikali kupitia REA imeleta maendeleo makubwa kwenye Sekta ya Nishati hususan kwenye usambazaji wa umeme vijijini katika kipindi cha miaka 15; akitolea mfano wakati alipokuwa Naibu Waziri wa Nishati mwaka 2008 ambapo bajeti ya REA ilikuwa shilingi bilioni tano pekee.
“Leo hii baada ya miaka 15 mkoa wa Morogoro pekee yake, unatekeleza Miradi ya umeme yenye thamani ya shilingi bilioni 91. Hii inaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuhakikisha Wananchi wa vijijini wanapata umeme kwa maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii.” alisema Mhe. Malima.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi, Thomas Mmbaga kutoka REA alisema wamewatambulisha rasmi wakandarasi wawili watakaofanya kazi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji 570 kwa mgawo wa kampuni ya Sagemcom Energy ambayo itasambaza umeme katika vitongoji 325 na kuunganisha wateja wa awali 11,399 katika wilaya ya Mvomero; Morogoro Vijijini na Gairo kwa gharama ya shilingi bilioni 48.4.
Mkandarasi wa pili ni kampuni ya China Railway No. 4 ambayo itasambaza umeme kwenye vitongoji 245 na kuunganisha wateja wa awali 8,649 katika wilaya ya Kilosa; Malinyi; Kilombero na Ulanga kwa gharama ya shilingi bilioni 42.5 ambapo kipindi cha utekelezaji kwa Mradi huo katika mkoa wa Morogoro ni miaka mitatu.
Naye Meneja wa TANESCO mkoa wa Morogoro, Mhandisi, Zawadi Macha alisema Shirika hilo limejipanga kikamilifu kusimamia utekelezaji wa Mradi huo kwa karibu ili kuhakikisha unatekelezwa kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Kampuni ya Sagemcom Energy, Bwana Calvin Manase alisema kampuni hiyo ina uzoefu mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme na imejipanga kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya miezi 34 licha mkataba kuwa miezi 36.
Manase aliongeza kuwa kampuni hiyo itatoa ajira kwa Wananchi (Wazawa) wa maeneo husika ili wanufaike moja kwa moja wakati wa utekelezaji wa Mradi huo. Aidha, ameipongeza REA kwa mpango wake wa kulipa malipo ya awali kwa wakandarasi akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya ujenzi wa Mradi huo.





.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...