
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewapongeza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa kusimamia vizuri mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Mbatakero na kubakiza ziada ya sh. milioni 4.33.
Ametoa pongezi hizo leo (Jumamosi, Februari 21, 2026) wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Weruweru mara baada ya kuzindua shule mpya ya sekondari ya Mbatakero, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro ambayo imejengwa kupitia mradi wa SEQUIP.
Viongozi waliopongezwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dionis Myinga, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Edmund Rutaraka, Mhandisi wa Wilaya, Arnold Matandiko na Afisa Elimu wa Wilaya sehemu ya sekondari, Margaret Muro.
Dkt. Mwigulu amesema ujenzi wa shule hiyo unatokana na dhamira ya dhati aliyonayo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuondoa kero zinazowasumbua wananchi. “Tunaposema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kuna watu huwa hawatuelewi. Lakini hawa waliokuwa wakitembea km. 18 kwenda na kurudi shuleni, wao na wazazi wao wanaelewa zaidi kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais wetu.”
“Kama mlivyosikia, Rais Dkt. Samia anapoelezwa kuna shida, anasema viongozi watatue changamoto hiyo, ndicho kilichotokea katika shule hii ambayo wanafunzi walilazimika kutembea umbali mrefu. Katika kipindi cha miaka minne, amejenga zaidi ya shule 1,300 za sekondari na amemaliza kabisa suala lililokuwa linaitwa chaguo la pili (second selection)”.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa shule hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Mhandisi Matandiko alisema ujenzi wake umegharimu sh. milioni 584.28 na kwamba uwepo wa shule hiyo utasaidia kuondoa adha waliyokuwa wanapata wanafunzi wa eneo hilo ya kutembea umbali km. 9 kwenda kwenda sekondari za Roo na Longoi ambazo ziko jirani na kijiji cha Mbatakero.
Alisema shule hiyo mpya ina madarasa nane, jengo la TEHAMA, jengo la utawala, maabara tatu za kemia, fizikia na baiolojia, kisima kimoja na matundu 10 ya vyoo.
Alisema wakati wa ujenzi kulikuwa na kazi zilizofanywa na wananchi ambayo thamani yake ni milioni 2.49 na hivyo kupunguza gharama, hali iliyowezesha wao kubaki na ziada ya sh. milioni 4.33 ambazo walishaomba kibali kwa Mkurugenzi zitumike kununua viti na meza za walimu ambavyo havikuwepo kwenye hela ya mradi
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Bomang’ombe hadi Kikavuchini kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 25.7 na kuzungumza na wananchi.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Hai, Mhandishi Kuya Francis alisema ujenzi wa barabara hiyo ulianza Agosti 05, 2024 na unatarajiwa kukamilika Mei 31, 2026. “Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 70 ambapo kazi zilizofanyika ni kuandaa tabaka la kwanza la barabara km 3.5, kuweka lami km 2.5, kujenga makutano ya barabara (roundabout) na kujenga mitaro na vivuko.
Alisema hadi kukamilika kwake mradi huo utagharimu sh. bilioni 2.99 na kwamba hadi sasa wameshapokea sh. milioni 569.73 katika awamu ya kwanza ambapo taratibu za kupokea sh. milioni 861.78 za awamu ya pili zinaendelea





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...