Na Fatma Jalala

Elimu na ushiriki wa wanawake katika ununuzi wa umma ni mhimili muhimu wa kukuza maendeleo ya kiuchumi na kujenga uchumi jumuishi nchini Tanzania, hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea kutekeleza Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023.

Sheria hiyo inazitaka taasisi zote za umma kutenga asilimia 30 ya ununuzi kwa ajili ya makundi maalum yanayohusisha wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wazee.

Hata hivyo, wanawake wajasiriamali na vikundi vya wanawake katika maeneo ya mijini na vijijini, ikiwemo wilaya ya Kinondoni, bado wanakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa taratibu za kushiriki katika zabuni za Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ya mwaka 2025, kati ya shilingi trilioni 14.9 zilizotumika kufanya ununuzi wa umma kupitia mfumo wa NeST, ni takribani shilingi bilioni 15 pekee zilikwenda kwa makundi maalum yote, kiwango ambacho ni chini ya asilimia moja ya thamani ya ununuzi wa umma.

Takwimu hizi zinaonyesha pengo kubwa kati ya malengo ya sera na utekelezaji halisi wa fursa kwa makundi maalum.

Ununuzi wa umma ni moja ya nguzo kuu za utekelezaji wa bajeti ya Serikali na chombo muhimu cha kuchochea uchumi. Kila mwaka Serikali hutumia zaidi ya asilimia 70 ya bajeti yake kufanya ununuzi wa bidhaa na huduma.

Ili fedha hizi ziwanufaishe na watu wa ngazi za chini pia, Serikali iliweka utaratibu wa kutenga angalau asilimia 30 ya thamani ya ununuzi wa umma kwa makundi maalum.

Lakini utafiti mbalimbali umeonyesha changamoto katika utekelezaji wa fursa hii. Kwa mfano, ripoti ya Africa Freedom of Information Centre (AFIC) kuhusu ununuzi jumuishi imeonyesha kuwa licha ya wanawake kumiliki sehemu kubwa ya biashara ndogo na za kati nchini, bado wanapata sehemu ndogo sana ya zabuni za Serikali kutokana na changamoto za uelewa mdogo wa taratibu za zabuni, urasimu na ukosefu wa taarifa sahihi.

Elimu ni kizuizi

Katika mahojiano na wanawake wajasiriamali wa Kinondoni, wengi walikiri kutokuwa na uelewa kuhusu fursa za ununuzi wa umma.

Blandina Daniel, mama lishe katika soko la Tandale, anasema: "Wanawake wengi hawajawahi kupata elimu kuhusu mfumo wa NeST wala ununuzi wa umma.”

Theresia Paschal Joseph, mjasiriamali katika soko la Magomeni, anasema: "Maisha ya ujasiriamali yamekuwa yakitegemea mapato ya kila siku bila matarajio ya kupanua biashara kutokana na kukosa taarifa na fursa."

Ingawa baadhi yao wanasema wamewahi kusikia juu ya fursa ya asilimia 30 kupitia vyombo vya habari, lakini hawajui hatua za kufuata ili kushiriki kikamilifu na wengi wao hawajasikia kabisa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizowahi kutolewa wakati wa makubaliano ya ushirikiano kati ya PPRA na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) mwaka 2024, changamoto ya ukosefu wa uelewa na elimu ya ununuzi wa umma imekuwa moja ya sababu kuu zinazokwamisha makundi maalum kunufaika na fursa hizi.

Wanawake wengi wanahitaji mafunzo ya vitendo yanayohusisha namna ya kuunda vikundi halali, kupata vyeti vya usajili, kuandaa nyaraka za zabuni na kutumia mifumo ya kielektroniki kama NeST.

Viongozi wa mitaa wakiri pengo la elimu

Baadhi ya viongozi wa Serikali za Mitaa akiwemo Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa Salum Kaponda wamekiri kuwa elimu kuhusu mfumo wa ununuzi wa umma bado haijawafikia wananchi kwa kiwango kinachohitajika.

Hali hii inaathiri uwezo wa wanawake kupata taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo.

Naye Diwani wa Kata ya Tandale, Abdulaziz Said, anasema hajawahi kupata taarifa rasmi kuhusu elimu ya mfumo huo.

Utafiti wa Africa Freedom of Information Centre (AFIC) ukiungwa mkono na PPRA, unaonyesha kuwa licha ya sheria ya Ununuzi wa Umma kutaka taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa makundi maalum, utekelezaji wake umekuwa mdogo sana.

Watafiti walibaini kuwa taasisi nyingi hazitii kikamilifu masharti hayo. Kwa mfano, bajeti ya mwaka 2021 baadhi ya taasisi hazikutenga kabisa bajeti ya ununuzi wa umma kwa ajili ya makundi haya.

Wajasiriamali wenyewe wanasema hali hii inasababishwa na mambo kadhaa ikiwemo ukosefu wa uelewa wa sheria, taratibu tata za usajili wa makundi katika mfumo wa NeST, na kutokuwepo kwa data ya kutosha juu ya utekelezaji wa sera hizi katika ngazi mbalimbali za serikali.

Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni kutoka PPRA hadi mwisho wa mwaka 2024, jumla ya makundi maalum 210 yalifanikiwa kushinda zabuni kupitia mfumo wa NeST, ikiwa na thamani ya takriban shilingi bilioni 9.85.

Katika hayo, vikundi vya wanawake vilishinda zabuni zenye thamani ya takriban shilingi bilioni 4 tu, na vikundi vya vijana vilishinda zabuni zenye thamani ya shilingi bilioni 3.9.

Hata hivyo, ingawa hizi ni takwimu chanya ikilinganishwa na hali ya awali, kiwango cha utekelezaji bado hakifikii kikomo cha asilimia 30 kinachotakiwa na sheria jambo linalobainika kuwa changamoto ya utekelezaji wa sera zinazolenga makundi maalum.

Kwa kifupi, uchambuzi huo unaonyesha kuwa ingawa serikali imeanzisha sheria ya ununuzi wa umma na mikakati kama makubaliano ya PPRA na NEEC, utekelezaji na ushiriki wa makundi maalum hasa wanawake bado unakabiliwa na vikwazo.

Makubaliano kati ya PPRA na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Uchumi (NEEC) yalisainiwa mwaka 2024 ili kuboresha uelewa na uwezo wa makundi maalum kushiriki kikamilifu katika zabuni za serikali. Sheria ya ununuzi inataka asilimia 30 ya zabuni ziwe kwa makundi kama wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wazee.

Hata hivyo, data ya utafiti inaonyesha kuwa utekelezaji umekuwa hafifu, taasisi nyingi bado hazitii kikamilifu vipaumbele vya asilimia 30, na sababu kubwa ni ukosefu wa uelewa wa taratibu za zabuni, ukosefu wa data bora ya makundi maalum, pamoja na kanuni tata za usajili za makundi katika mfumo wa NeST. Pia, sheria hiyo inahitaji makundi kuwa na muundo maalum wa kikundi, jambo lililozua usumbufu kwa wafanyabiashara binafsi wakiwemo wanawake wanaoishi maeneo tofauti na wenye biashara za mtu mmoja.

Umuhimu wa ushiriki wa wanawake

Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa ushiriki wa wanawake katika ununuzi wa umma una faida kubwa kwa uchumi wa taifa.

Unasaidia kuongeza kipato cha wanawake na familia zao, kupunguza umasikini wa kaya, kukuza ujasiriamali na kuongeza pato la Taifa kupitia kodi.

Wanawake wengi wana ujuzi na ubunifu mkubwa wa kuzalisha bidhaa na huduma bora kwa gharama nafuu. Kupitia ununuzi wa umma, wanaweza kupata soko la uhakika na kukuza biashara zao kwa kiwango kikubwa zaidi.

Ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika ununuzi wa umma, ni muhimu kuimarisha utoaji wa elimu na mafunzo ya vitendo kuhusu taratibu za zabuni, usajili wa biashara na vikundi, matumizi ya mfumo wa NeST, na ushirikiano wa taasisi husika.

Wanawake wanapaswa kuunda vikundi halali au kusajili biashara zao, kusajili kampuni kupitia BRELA, kujiunga na vyama vya ushirika au SACCOS, pamoja na kujisajili katika mfumo wa NeST. Ni muhimu pia kuwa na nyaraka halali kama cheti cha usajili, TIN na akaunti ya benki ya kikundi au biashara

Pamoja na uwepo wa sheria na sera rafiki, bado kuna haja ya kuongeza elimu na uhamasishaji kwa wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu katika ununuzi wa umma.

Ushirikishwaji wa wanawake katika ununuzi wa umma si hisani, bali ni haki ya kisheria na mkakati muhimu wa maendeleo ya Taifa.

Kama watajengewa uwezo kupitia elimu sahihi, mafunzo ya vitendo na ushirikiano wa taasisi husika, wanawake wana uwezo mkubwa wa kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya familia na jamii kwa ujumla.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...