Tume ya Ushindani (FCC) imesema itaendelea na mchakato wa marekebisho ya sheria zake kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa walaji, kudhibiti bidhaa bandia na kuhakikisha kunakuwepo ushindani wa haki unaochochea ukuaji wa uchumi na ajira nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, wakati akifungua semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Ngasongwa amesema marekebisho hayo yanalenga kumlinda mlaji dhidi ya bidhaa zisizo na ubora, matangazo ya upotoshaji pamoja na vitendo vinavyokwenda kinyume na misingi ya ushindani wa haki sokoni.
Amesema moja ya vipaumbele vya Tume hiyo ni kuimarisha udhibiti wa bidhaa bandia zinazoingia sokoni, akibainisha kuwa bidhaa hizo huathiri afya za wananchi, hupunguza mapato ya Serikali na kuwanyima wafanyabiashara halali fursa ya kukuza biashara zao.
“Jukumu letu ni kuhakikisha uchumi unakua kwa misingi ya ushindani wa haki. Matokeo yake ni kuongezeka kwa uwekezaji na ajira kwa wananchi,” alisema Ngasongwa.
Aidha, amesema FCC itaendelea kukutana mara kwa mara na waandishi wa habari pamoja na wadau mbalimbali kwa lengo la kutoa taarifa sahihi kuhusu majukumu yake na kusikiliza changamoto za wananchi ili kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.
Katika hatua nyingine, amesema kuna maboresho yanayofanyika kupitia TANOGA — muunganiko wa taasisi za Serikali za udhibiti pamoja na mawakala wa forodha — kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa bidhaa zinazoingia nchini.
Ngasongwa ameongeza kuwa taasisi hizo zinaelekea kuingia katika mfumo wa kidijitali utakaopunguza mwingiliano wa moja kwa moja kati ya watumishi na wateja, hatua itakayosaidia kuongeza uwazi, kupunguza urasimu na kudhibiti mianya ya vitendo visivyo vya kiadilifu.
FCC imeahidi kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali pamoja na sekta binafsi ili kuhakikisha mazingira ya biashara nchini yanabaki kuwa salama, yenye ushindani wa haki na yenye manufaa kwa wananchi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa, akizungumza wakati akifungua semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari iliyoandaliwa na Tume hiyo, iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Februari 24, 2026.
Makamu wa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi Habari Mkoa wa Dar ea Salaam (DARPC) Mary Geofrey akitoa maelezo kuhusiana na semina ya FCC itavyochochea ushindani wa soko ,jijini Dar es Salaam.
Semanina ikiendelea
Picha pamoja ya wafanyakazi wa FCC na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC Khadija Ngasongwa katika Semina ya Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.
Picha pamoja ya waandishi wa Habari na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC Khadija Ngasongwa katika Semina ya Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...