Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amesema kuwa uongozi wa mkoa umeweka mkakati mahsusi wa kujenga mfumo thabiti na shirikishi wa kuwawezesha vijana kiuchumi, unaojumuisha mafunzo ya ujuzi, upatikanaji wa mitaji pamoja na kuwatafutia masoko ya uhakika kwa bidhaa na huduma zao.
Akizungumza Februari 20, 2026 katika hafla ya ugawaji wa vitendea kazi kwa wajasiriamali iliyofanyika katika Ukumbi wa SIDO, Mhe. Kheri amesema hatua hiyo ni sehemu ya dira ya mkoa kuifanya Iringa kuwa kitovu cha uzalishaji na uongezaji thamani wa rasilimali zilizopo ndani ya mkoa.
Vitendea kazi hivyo vimetolewa kupitia Mradi wa SET (Skills for Employment Tanzania) unaotekelezwa na Swisscontact, ukiwa na lengo la kuwawezesha vijana waliopatiwa mafunzo kuanzisha au kupanua shughuli zao za uzalishaji kwa tija zaidi.
Mhe. Kheri amefafanua kuwa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki yanayochochea ushirikiano kati ya sekta ya umma, sekta binafsi na wadau wa maendeleo, jambo linalorahisisha utekelezaji wa mipango ya kuwainua vijana kiuchumi.
Aidha, amebainisha kuwa mkoa wa Iringa una fursa kubwa kutokana na ardhi yake yenye rutuba kwa shughuli za kilimo, rasilimali za misitu pamoja na sekta ya utalii inayokua kwa kasi, na kusisitiza kuwa rasilimali hizo zikitumika ipasavyo zinaweza kuwa chachu ya ajira na ustawi wa vijana wengi zaidi.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...