Na Seif Mangwangi , Michuzi TV, Arusha.

Mahakama ya Afrika ya Haki za  Binadamu na Watu (AfCHPR) imemchagua Jaji Blaise Tchikaya wa Serikali ya Jamhuri ya watu wa Kongo (Brazzaville) kuwa Rais mpya wa Mahakama hiyo akichukua nafasi ya Jaji Dkt. Modibo Sacko aliyemaliza muda wake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Kwa vyombo vya habari na Mahakama hiyo Jaji Tchikaya amechaguliwa katika kikao cha majaji kilichofanyika Februari 23, 2026.

Taarifa hiyo imesema Rais mpya   atahudumu kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa Rais anayeondoka, ambaye alichaguliwa tarehe 2 Juni 2025 kwa kipindi cha miaka miwili huku, Jaji Sacko akiendelea kusalia katika benchi la Mahakama kama Jaji.

Katika hotuba yake ya kuaga, Jaji Sacko alitoa shukrani za dhati kwa Majaji wenzake, Msajili, wafanyakazi na wadau wote wa Mahakama kwa ushirikiano na uungwaji mkono waliompa wakati wa uongozi wake.

Katika hotuba yake baada ya kuchaguliwa Rais mpya Jaji Tchikaya amesema amepokea jukumu hilo kwa heshima kubwa na dhamira ya kuendeleza misingi ya Mahakama akisisitiza kuwa wakati Mahakama ikijiandaa kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, ni muhimu kutafakari mafanikio yaliyopatikana na kukabiliana na changamoto zilizopo ili kuimarisha zaidi ulinzi wa haki za binadamu barani Afrika.

Kwa niaba ya Mahakama, alitoa pongezi na shukrani kwa Jaji Sacko kwa uongozi wake thabiti na mchango wake katika kuimarisha taasisi hiyo muhimu ya Umoja wa Afrika.

Kufuatia uchaguzi huo, ofisi mpya ya uongozi sasa inaundwa na Jaji Blaise Tchikaya kama Rais na Jaji Bensaoula Chafika wa Algeria kama Makamu wa Rais.

*Wasifu wa Rais Jaji Blaise Tchikaya*

Rais Jaji Blaise Tchikaya ni Profesa wa sheria za umma za kimataifa na haki za binadamu mwenye uzoefu mpana wa kitaaluma.

Alichaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama hiyo Julai 2018 kwa muhula wa miaka sita na aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo kuanzia Juni 2021 hadi Julai 2023.

Kwa upande wake Makamu wa Rais Jaji Bensaoula Chafika ana Shahada ya Uzamivu katika Sheria ya Umma na amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu katika mahakama na utawala nchini Algeria pamoja na kuwa mhadhiri na mshauri wa masuala ya sheria.

Alichaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama hiyo mwaka 2017 na kuchaguliwa tena mwaka 2023 kwa muhula wa pili na Juni 2, 2025 alichaguliwa tena kwa muhula wa miaka miwili.

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ni chombo cha Umoja wa Afrika kilichoanzishwa na Nchi Wanachama wake kwa lengo la kulinda na kuimarisha haki za binadamu na watu barani Afrika.

Mahakama hiyo inaundwa na Majaji 11 wanaochaguliwa kwa uwezo wao binafsi na hukutana mara nne kwa mwaka katika vikao vya kawaida pamoja na vikao vya ziada pindi inapohitajika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...