Na FARIDA MANGUBE, MOROGORO.


Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inampango kuanzisha zaidi ya vituo 1,000 vya kuhifadhi mashine za kilimo ili kurahisisha upatikanaji wake kwa wakulima na kuongeza uzalishaji.

Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu (Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula) wa Wizara ya Kilimo, Profesa Peter Msoffe, mjini Morogoro alipomwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo katika jukwaa la kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania na Japan kupitia Japan International Cooperation Agency (JICA), kwa kushirikiana na Sokoine University of Agriculture (SUA).

Profesa Msoffe amesema mafanikio ya mageuzi ya kilimo hayawezi kupatikana bila kuwekeza katika kilimo cha kisasa kinachotumia mashine badala ya kutegemea nguvu kazi ya mikono.

Ameleza kuwa vituo hivyo vitahusika na kuhifadhi na kufanya matengenezo ya mashine, pamoja na kuhakikisha zinapatikana kwa urahisi kwa wakulima.

Amesema dhamira ya Serikali ya kuboresha kilimo si ya maneno bali ni ya vitendo, akibainisha kuwa tayari hatua za kuanzisha vituo hivyo zimeanza sambamba na utoaji wa ruzuku ya mbolea na pembejeo mbalimbali kwa wakulima.

Akizungumzia uzoefu wa Japan katika kuendeleza kilimo cha kisasa, Profesa Msoffe alisema Tanzania ina mengi ya kujifunza, akifananisha ushirikiano huo na darasa muhimu kwa wataalamu wa kilimo nchini.

Jukwaa hilo, ambalo limekuwepo kwa takribani miaka minne, linawakutanisha wataalamu kutoka Tanzania na Japan kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya teknolojia na mashine katika sekta ya kilimo.

“Kama mnavyofahamu, Tanzania inapitia mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo. Baada ya kupitishwa kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, nchi imejipanga kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kufikia uchumi wa takribani dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050, huku kipato cha mwananchi kikitarajiwa kufikia wastani wa dola 7,000,” alisema.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA nchini Tanzania, Ara Hitoshi, alisema ushirikiano kati ya JICA na SUA ulianza mwaka 2022 ukiwa na lengo la kushirikiana katika maendeleo ya sekta mbalimbali, hususan kuwawezesha vijana.

Amesema kilimo ni sekta muhimu kwa uchumi wa Tanzania na kupitia jukwaa hilo vijana watanufaika kwa kujifunza namna Japan inavyotumia mashine na teknolojia za kisasa katika uzalishaji badala ya kutegemea kilimo cha mazoea.

“Nafikiri kilimo ni sekta muhimu kwa Tanzania. Tunapenda kushirikiana katika programu hii ili wataalamu wa Japan na Tanzania wabadilishane uzoefu, hususan kwa kuwalenga vijana katika matumizi ya teknolojia za kisasa,” alisema.

Afisa Mwandamizi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Edwin Konzo, alisema ili kufikia malengo ya Dira ya 2050 kuna haja ya kufanya mapitio ya sera mbalimbali, ikiwemo Sera ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1996, ili iendane na mahitaji ya sasa.

Amesema sekta ya kilimo ni injini muhimu ya mabadiliko ya kiuchumi na mafanikio yake yanategemea matumizi ya teknolojia na ubunifu.

“Mkutano huu unalenga kujifunza kutoka kwa teknolojia zilizotumiwa na Japan katika mageuzi ya kilimo, ili wataalamu wetu waweze kutumia maarifa hayo kuboresha uzalishaji, kuendeleza mbegu zenye ustahimilivu na kuongeza faida kwa wakulima,” alisema.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa SUA (Utawala, Fedha na Mipango), Profesa Amandus Muhairwa, alisema jukwaa hilo linatoa fursa kwa Watanzania kujifunza kutoka kwa Wajapani kuhusu uhandisi na teknolojia katika kilimo.

Ameongeza kuwa wakati vijiji vingi vikibadilika na kuwa miji, eneo la ardhi linalopatikana kwa kilimo linapungua, hivyo kuna haja ya kuongeza tija katika uzalishaji, si tu katika kilimo bali pia katika sekta ya ufugaji.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...