Na Mwandishi wetu Simanjiro


MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Simanjiro James Ole Millya kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Kaleiya Mollel akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika mji mdogo wa Orkesumet amesema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Ole Millya kushika nafasi hiyo.

"Tangu dunia iumbwe ni mara ya kwanza Simanjiro kutoa Naibu Waziri hivyo tumpe ushirikiano wa kutosha ili aweze kuitumikia vyema nafasi hiyo ambayo Rais Samia ameona inamfaa katika kuitumikia," amesema Kaleiya.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mwanjaa Jacob amesema Ole Millya amewapa heshima kubwa watu wa Simanjiro hivyo watamuunga mkono ili aitumikie nafasi hiyo ipasavyo.

"Mbunge wetu ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, hii ni heshima kubwa tumepewa wana Simanjiro tunatarajia wote tumuunge mkono mbunge wetu ili atimize vyema majukumu yake," amesema Mwanjaa.

Diwani wa Kata ya Mirerani Salome Mnyawi amesema kupitia nafasi hiyo anaimani kubwa Simanjiro itapiga hatua kubwa zaidi kwani wanaye mbunge ambaye yupo Serikali kupitia nafasi ya Naibu Waziri.

"Kwa sasa mbunge wetu yupo jikoni anaweza akafanikisha maendeleo hivyo tumpe ushirikiano mkubwa wana Simanjiro," amesema Salome.

Hata hivyo, Ole Millya akizungumza kwenye kikao cha baraza hilo amewashukuru madiwani hao kwa kumpa pongezi hizo na ushirikiano katika nafasi yake.

"Kipekee nimshukuru Mhe DC Simanjiro mwalimu Fakii Raphael Lulandala, DED Simanjiro Gracian Max Makota, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe Kaleiya na viongozi wote kwa namna wanavyonipa ushirikiano wa kutosha," amesema Ole Millya.

Amesema japokuwa hivi sasa mara nyingi anaishi Dar es salaam na Dodoma ila anawasiliana kwa karibu na viongozi hao wa Simanjiro kwa njia ya simu hata usiku wa manane kwa ajili ya maendeleo ya eneo hilo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...