-SERIKALI IMEENDELEA KUCHUKUA HATUA ZA MAKUSUDI ZA KUIMARISHA UHURU WA MAHAKAMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema kwa kutambua umuhimu wa Mahakama katika ujenzi wa Taifa, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi katika kuimarisha uhuru wa Mahakama ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake kikamilifu na kuchochea ustawi na maendeleo ya Taifa.

 Makamu wa Rais amesema hayo, wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli, Jijini Dodoma. Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, kuimarisha rasilimali watu, kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama, na kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi, hususan kupitia mpango wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo kwa Kata zote nchini zisizo na  Mahakama za Mwanzo.

Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwamba, uhuru wa Mahakama usitumike kama sehemu ya kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki. Amesema uhuru huo ni dhamana ya kutenda haki kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi.

 Makamu wa Rais amesema Mahakama ina wajibu muhimu wa kulinda utawala wa sheria, kusimamia utekelezaji wa mikataba, kulinda rasilimali za Taifa, na kuhakikisha kuwa maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wote kwa usawa.

 Ameongeza kwamba Mahakama ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 kwa Kuendelea kulinda haki na misingi ya Katiba, Kuhakikisha migogoro ya kiuchumi, kibiashara na kijamii inatatuliwa kwa haraka na kwa haki, Kujenga imani ya wananchi na wawekezaji katika mfumo wa kisheria wa nchi, Kukuza uwajibikaji na nidhamu katika utumishi wa umma na sekta binafsi pamoja na Kudumisha amani na mshikamano wa Kitaifa, ambao ni msingi wa maendeleo endelevu.

 Pia amesema ni muhimu Mahakama, Kuzuia migogoro inayoweza kuwa chanzo cha migawanyiko ya kijamii au kisiasa, Kuharakisha utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo kwa kutoa tafsiri ya kisheria iliyo wazi na thabiti, Kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuheshimu sheria, haki na taasisi za umma, Kuchangia katika mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka pamoja na Kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa kwa kuwahakikishia ulinzi wa haki zao za kisheria.

 Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewaasa viongozi, wanasiasa, wanaharakati na wananchi mbalimbali kuheshimu tume iliyoundwa na Rais ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa kuacha kuongelea masuala hayo nje ya mfumo wa kisheria.  Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo kufuatia maombi ya Rais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Boniface Mwabukusi ambaye aliomba Viongozi kuacha kuzungumzia suala hilo ambalo limekuwa likiwaumiza wananchi.

 Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju amesema Mahakama inaendeleza na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Mahakama ili kuimarisha ufanisi. Amesema kwa sasa Mahakama inajenga mfumo unaotumia Akili Unde (AI) kwaajili ya kurekodi mwenendo wa kumbukumbu za mashauri na hukumu Mahakamani.

 Amesema katika mfumo huo, Jaji, Hakimu, Wakili na Shahidi wanapozungumza mahakamani mfumo huo utatafsiri lugha iliyotumika na kuiandika kwa lugha iliyokuwa imechaguliwa kuandika kwa wakati huo huo. Ameongeza kwamba mfumo huo utakapoanza kutumika utaimarisha ufanisi wa utendaji wa Mahakama kwani kuchukua kumbukumbu za mwenendo wa mashauri Mahakamani kwa kuandika kwa mkono au kompyuta kunachelewesha na wakati mwingine kupotosha.






Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...