Na Diana Byera,Karagwe
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Devotha Daniel, ametoa msaada wa Sh. 1,000,000 kwa mtoto Grecseous Raphael mwenye umri wa miezi 4, mkazi wa Kata ya Kihanga, Wilaya ya Karagwe, anayesumbuliwa na uvimbe kichwani
Lengo la msaada huo ni kumuwezesha mtoto huyo kupelekwa Hospitali ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya upasuaji.
Mbunge Devotha Daniel ametoa msaada huo ikiwa ni katika kipindi cha kuendelea kusambaza tabasamu kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, amesema alipata taarifa za mtoto huyo kupitia matangazo ya kituo cha redio ya jamii cha Fadeco Radio, ambapo mama wa mtoto alikuwa akiomba msaada kwa wasamaria wema.
“Baada ya kusikia taarifa hizo, niliguswa na kuamua kufika moja kwa moja kwa familia ya mtoto kwa ajili ya kuona hali halisi na kutoa mchango wangu.”
Mbali na msaada huo wa fedha ameahidi kugharamia bima ya afya kwa familia nzima ya mtoto huyo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na ulinzi wa matibabu.
Kwa upande wake, mama wa mtoto Swaumati Sijaji amemshukuru Mbunge huyo kwa kufika nyumbani kwao na kuwafariji pamoja na kutoa msaada huo ambao utasaidia kumpeleka mtoto waoHospitali ya Kanda ya Bugando kufanyiwa upasuaji wa uvimbe huo.
Hata hivyo familia ya mtoto huyo imesema msaada huo umewapa matumaini mapya ya kuona mtoto wao anapatiwa matibabu stahiki na kurejea katika hali ya kawaida.Hawakutarajia kupata msaada kwa haraka kiasi hicho huku wakimuahidi kumuombea Mbunge huyo ili aendelee kuwahudumia wananchi kwa moyo wa huruma.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Karagwe Georgiana Mkapapa amesema kitendo hicho kinaonesha namna Mbunge huyo alivyo karibu na wananchi wake, na kuwataka wanawake na wananchi kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono na kumuamini katika jitihada zake za kuwatumikia na kuwaletea maendeleo.


.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...