Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Miji na Vijiji kutoka TAMISEMI, Rachel Kaduma, amesema utekelezaji wa Mradi wa Green and Smart Cities unaendelea katika hatua mbalimbali ukiwa na lengo la kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha huduma za kijamii katika maeneo ya mijini.

Akizungumza leo Februari 25, 2026 Jijini Dar es Salaam katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo , Kaduma alisema mradi unahusisha ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya kiuchumi ikiwemo maeneo ya uvuvi, pamoja na kuwajengea uwezo vijana kupitia mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA.

Alifafanua kuwa mafunzo hayo yanawawezesha vijana kupata ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa katika sekta mbalimbali za uchumi.

“Lengo la mradi huu si tu kuboresha miundombinu, bali pia kuhakikisha miji inakuwa safi, salama na yenye mazingira rafiki kwa wananchi. Huduma muhimu zinaimarishwa ili wananchi wapate huduma bora kwa urahisi,” alisema Kaduma.

Aidha, alibainisha kuwa kikao hicho kimeandaliwa kujadili changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi na kutoa mapendekezo yatakayowasilishwa kwa viongozi wa juu kwa ajili ya maamuzi.

“Tunapitia changamoto mbalimbali, lakini pia tunapata fursa ya kubadilishana uzoefu kati ya wadau. Wale waliofanikiwa wanashirikisha wenzao mbinu walizotumia kuboresha utekelezaji,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mratibu wa Programu ya Green and Smart Cities katika Manispaa ya Ilemela, Ahmed Sakif, alisema programu hiyo inafadhiliwa na Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alieleza kuwa mradi ulianza mwaka wa fedha 2022/2023 na unatekelezwa katika halmashauri mbalimbali zikiwemo Jiji la Mwanza na Jiji la Tanga.

Sakif alitaja maeneo makuu matatu ya utekelezaji kuwa ni msaada wa kibajeti kwa halmashauri, uboreshaji wa miundombinu ya umma kama masoko na mialo ya samaki, pamoja na uhifadhi wa mazingira na rasilimali maji.

Aliongeza kuwa kupitia mradi huo, vijana zaidi ya 600 wamepata mafunzo ya ufundi stadi na wanatarajiwa kuunganishwa na fursa za mitaji ili kuanzisha shughuli za kujiajiri.

Wadau wa mradi huo wamesema hatua zilizofikiwa zinaonesha mafanikio, huku wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya maendeleo na wananchi ili kuhakikisha mradi unaleta matokeo chanya.

Akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Ulaya, Ulrik Jorginsen alisema ujumbe wa EU nchini Tanzania unatekeleza programu hiyo kwa kushirikiana na serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu.

Alisema programu inalenga kusaidia maendeleo endelevu katika miji ya Tanzania, hususan miji ya sekondari, kwa kuboresha huduma muhimu kama maji safi na usafi wa mazingira.

“Kazi kubwa imefanyika katika maeneo ya Unguja na Pemba, hususan katika upanuzi wa miundombinu ya maji na usafi wa mazingira,” alisema.

Aliongeza kuwa awamu zinazofuata za mradi zinaendelea, huku mipango ikiwekwa ya kuanzisha miradi kama hiyo katika Jiji la Tanga ili kuboresha huduma za msingi kadri miji inavyokua.

“Mbali na sekta ya maji, programu pia inashughulikia maendeleo ya masoko na biashara ndogo ndogo kupitia mpango wa Inclusivity,” alisisitiza.

Kupitia mpango huo, vijana na wanawake wanapewa fursa ya kuimarisha biashara zao na kuunganishwa na masoko, hatua inayolenga kukuza uchumi wa ndani na kuongeza ajira.

Jorginsen alihitimisha kwa kusisitiza kuwa ujenzi wa uwezo wa taasisi za ndani ni muhimu ili ziweze kusimamia miradi hiyo kwa uendelevu hata baada ya programu kukamilika.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...