Na Said Mwishehe
KITENDO cha kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba Multaza Ally Mangungu jana baada ya kumalizika kwa mechi kati ya SIMBA na ESPERANCE kimetuudhi mashabiki wa soka Tanzania naamini hata Duniani.
Sio kitendo cha kiungwana hata kidogo kilichofanywa na baadhi ya mashabiki wa Simba ambao kupitia video mjongeo(video fupi)wameonekana wakimshambulia Mangungu na mmoja wa mashabiki akionekana kabisa akimpiga ngumi
Ni mambo ya hovyo kabisa, ni mambo ya kijinga na ni ushamba uliopiilitiza. Ni ushabiki wa kizamani na wengine tulishasahau matukio ya Viongozi wa soka hapa Tanzania kushambuliwa.
Tujiulize kwa akili ya kawaida kosa la Mangungu ni lipi ?Ile sare ya 2-2 ambayo imepatikana jana Mangungu anahusika vipi?
Alikuwepo ndani ya Uwanja akicheza? Yeye ndiye aliyetoa ile pası ya hovyo iliyosababisha ESPERANCE wapate goli la kwanza kabla ya kufunga goli la pili na kufanya mchezo kumaliza kwa sare ya 2-2.
Najaribu kujiuliza waliomshambulia Mangungu wanajua majukumu yake pale SIMBA? Wanajua mipaka yake ya kutekeleza majukumu yake inaanzia wapi na kuishia wapi?
Unamshambuliaje kiongozi ambaye yeye sio kocha,hapangi timu wala hakai benchi la ufundi? Sawa Mangungu yuko pale SIMBA kwa nafasi ya Mwenyekiti hebu tujiulize yuko peke yake?
Hakuna viongozi wengine pale SIMBA? Kwanini kila siku yeye? SIMBA ikifanya vizuri Mangungu wala hakuna anayemtaja hata kumpongeza lakini timu ikifungwa basi Mangungu .
Wana Simba na hasa mashabiki OYA OYA acheni mambo ya kijinga.Simba ni ya Wana Simba wote. Kumekuwa na tabia siku hizi kwa baadhi ya mashabiki wanajifanya wenyewe ndio wanaumizwa sana na SIMBA kufanya vibaya, hovyo kabisa.
Timu ikishinda wako kimya ,ikifungwa wanakimbilia mitandaoni kutukana viongozi na wachezaji. Ni mashabiki wa hovyo sana.
Ni mashabiki wasiojitambua.Tunafahamu Simba ina wanachama, mashabiki na wapenzi ambao wanaipenda timu yao, wanawapenda viongozi wao na wanawapenda wachezaji.
Wao wapo na timu bila kujali nyakati wanazopitia. Ni SIMBA hii na Mangungu akiwa Mwenyekiti imefanya makubwa katika soka la Tanzania ,soka la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Nani ambaye hajui ukubwa wa Simba Afrika? Iko nafasi ya tano kwa ubora.Katika mafanikio hayo ya Simba huwezi kuliacha jina la Mangungu kwani kama kiongozi ana mchango wake katika mafanikio hayo.
Simba imekuwa bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Mara nne mfululizo na sio miaka mingi iliyopita,sasa kwanini Wana Simba hasa ninyi mashabiki uchwara mnajisahaulisha.
Mangungu amepatikana kupitia uchaguzi mkuu wa Simba kama humtaki wakati ukifika kachukue fomu ugombee au kamchukulie fomu huyo unayemuona anafaa kuwa Mwenyekiti wa Simba.
Haya mambo ya kumshambulia hakuna anayefurahishwa. Niliombe Jeshi la Polisi kuchukua hatua dhidi ya wale wote ambao wameonekana wakimshambulia Mangungu.
Kupitia video zinazosambaa mtandaoni wale wote wakamatwe na wachukukuliwe hatua. Kuna haja ya kukomesha tabia hii kabla haijakomaa na kuharibu soka la Tanzania, kukatisha tamaa viongozi.
Ni wakati wa wadau wa soka kukemea tabia hii.Katika Ulimwengu wa soka wanaamini katika soka ni burudani,soka ni furaha na kubwa zaidi soka inaongozwa na Fair Play.
Mwenyekiti Mangungu pole, tunakuombea kwa Muumba wa mbingu na ardhi aendelee kukupa afya na uzima.
Tunakuombea kwa Mungu aendelee kukupa hekima ,busara na maarifa katika kuendelea kutekeleza majukumu yako ndani ya Klabu ya Simba.
Wadau wa soka nchini tunaheshimu na kutambua mchango wako.Ila nikunong’oneze kuna baadhi ya Wana Simba wenzako ndio wanaeneza propaganda chafu ili kukuchafua .
Kuwa makini kwani kwa ile video ya jana unaona kabisa ni kama kuna watu nyuma yao waliotengeneza tukio lile ili ushambuliwe,unyanyasike uwanjani.Pole Mangungu but tunajua wewe ni kiongozi imara na hivyo utabaki kuwa imara.
Simu 0713833822.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...