Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), amekipongeza Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa kuweka mipango na mikakati inayotembea katika maono ya  dira Taifa ya mwaka 2025-2050, ikiwemo mageuzi ya Kidijitali na Utafiti na Maendeleo.

Mhe. Luswetula ameyasema hayo Februari 06, 2026 katika mahafali ya 27 ya IAA duru ya Pili, yaliyofanyika Ngurodoto jijini Arusha akimwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Omar Mussa.

Mhe. Luswetula amesema mipango inayofanywa na IAA ya kuboresha miundombinu ya TEHAMA, mifumo ya kujifunzia kwa njia ya mtandao hususani kwa Shahada ya Uzamili (master’s degree), usimamizi wa kitaaluma ni nguzo muhimu katika kuongeza ufanisi na ushindani wa Chuo kitaifa na kimataifa.

“Mageuzi ya Kidigitali ni kichocheo muhimu cha maendeleo hususani katika kuboresha ukuaji wa uchumi na kuimarisha huduma za jamii ikiwemo elimu. Serikali inatambua na kupongeza juhudi za IAA katika kuwekeza kwenye mifumo ya kidigitali”, amesema Mhe.Luswetula.

Aidha, ameipongeza IAA kwa kuendelea kuzalisha wataalam mahiri wa fedha, uhasibu, uchumi, kodi, utalii, usimamizi biashara, benki, ununuzi na ugavi, masoko, bima, TEHAMA na nyingine nyingi; ambao wamekuwa mhimili muhimu katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, usimamizi wa fedha za umma, sekta binafsi, taasisi za kifedha na miradi ya maendeleo.

Vile vile, Mhe.Luswetula awasisitiza wanafunzi na wahitimu wa Shahada ya Uzamili kuimarisha zaidi tafiti zao za kitaaluma kwa kuzielekeza katika kutoa majibu ya changamoto halisi zinazoikabili jamii na Taifa letu, ikiwemo masuala ya usimamizi wa fedha za umma, ukuaji wa uchumi jumuishi, ajira, ubunifu, na matumizi sahihi ya teknolojia.

Mkuu wa Chuo IAA, Prof. Eliamani Sedoyeka amesema IAA wanajivunia kuwa miongoni mwa taasisi za elimu ya juu nchini zinazotekeleza mwelekeo wa Kitaifa wa kupanua upatikanaji wa elimu ya juu kwa kuanzisha na kuimarisha mfumo jumuishi wa utoaji wa shahada ya Uzamili (Master’s degree) unaochanganya masomo ya ana kwa ana darasani (Physical classes) na ya mtandaoni  kwa wakati mmoja yaani ‘blended mode’.

Prof Sedoyeka ameongeza kuwa IAA imeweka mkakati  kuwawezesha wahadhiri wengi zaidi kusomea Shahada ya Uzamivu, ili kukidhi ongezeko la idadi ya wanafunzi wa Uzamili linaloendelea kushuhudiwa kila mwaka, ambapo jumla ya wahadhiri 115 wamepelekwa kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika vyuo mbalimbali nchini na nje ya nchi katika mwaka wa masomo 2025/2026.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo IAA, Dkt. Mwamini Tulli amesema Katika mahafali ya 27 duru hii ya pili  jumla ya wahitimu 2,250 kati yao wanaume ni 1,369 sawa na asilimia 60.8 na wanawake 881 sawa na asilimia 39.2 wametunukiwa Shahada ya Uzamili ya Chuo cha Uhasibu Arusha(IAA) katika fani 15.








 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...