Na Avila Kakingo, Michuzi TV
MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali imeendelea kuimarisha usalama wa usafiri wa majini na kukuza sekta ya utalii kwa kasi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza kuhusu hatua zinazochukuliwa kulinda maisha ya wananchi na mali zao, Msigwa amesema Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imewekeza kwa kiasi kikubwa katika mifumo ya utafutaji na uokoaji majini ili kuhakikisha dharura zinashughulikiwa kwa haraka na kwa ufanisi.
Amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 na nusu ya mwaka 2025/26, Serikali imekamilisha ujenzi wa Kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokoaji cha Kikanda (MRCC) katika Ziwa Victoria, mkoani Mwanza, kwa kushirikiana na Serikali ya Uganda. Kituo hicho kitaimarisha uratibu wa operesheni za utafutaji na uokoaji, matumizi ya mifumo ya kisasa ya mawasiliano na TEHAMA pamoja na utoaji wa tahadhari za hali ya hewa, hatua itakayoongeza usalama katika shughuli za usafiri ndani ya Ziwa Victoria.
Aidha, kupitia Wakala wa Usafiri wa Majini Tanzania (TASAC), Serikali imenunua boti maalum ya wagonjwa (Ambulance Boat) kwa ajili ya Ziwa Victoria ambayo tayari imewasili na iko tayari kutoa huduma.
Boti hiyo ni kama hospitali inayotembea majini, itakayosaidia kuwahudumia wananchi waishio visiwani na maeneo ya mwambao.
Pamoja na hilo, Serikali imenunua boti moja ya utafutaji na uokoaji kwa ajili ya Ziwa Tanganyika, boti mbili kwa Ziwa Victoria, na boti moja kwa ukanda wa Bahari ya Hindi mkoani Tanga.
Hatua hii imeongeza uwezo wa taifa kukabiliana na ajali na majanga ya majini kwa wakati.
Katika kuimarisha mawasiliano ya dharura, Wizara inaendelea na ujenzi wa minara mitatu ya mawasiliano katika Ziwa Victoria, ambapo mnara wa Kisiwa cha Soswa na wa Kisiwa cha Kunene umefikia asilimia 50 ya utekelezaji.
Mradi huo unalenga kuboresha mawasiliano ya dharura, tahadhari za hali ya hewa na uratibu wa shughuli za uokoaji.
Msigwa ameeleza kuwa uzoefu uliopatikana katika Ziwa Victoria utatumika kupeleka miradi kama hiyo katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa, ili kuhakikisha maziwa yote makuu nchini yanakuwa salama kwa usafiri wa majini.
Wakati huo huo Msigwa alizungumzia upande wa utalii, nakusema Tanzania inaendelea kung’ara kimataifa kutokana na rasilimali zake za kipekee zikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mlima Kilimanjaro, eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa Ruaha, Hifadhi ya Taifa Mikumi pamoja na Zanzibar.
Amebainisha kuwa mwaka 2024 Tanzania ilipokea watalii wa nje 2,141,895 ikilinganishwa na watalii 2,294,495 mwaka 2025. Watalii wa ndani waliongezeka kutoka 3,218,352 mwaka 2024 hadi 3,610,960 mwaka 2025.
Jumla ya watalii (ndani na nje) iliongezeka kutoka 5,360,247 mwaka 2024 hadi 5,905,455 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 10.2.
Mapato ya utalii nayo yamepanda kutoka dola za Marekani milioni 1.3 mwaka 2021 hadi dola milioni 3.9 mwaka 2024, hali inayoonesha mafanikio makubwa ya mikakati ya kuitangaza Tanzania kimataifa na kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, reli na barabara.
Msigwa amesema mafanikio hayo yamechangiwa pia na jitihada za kuitangaza Tanzania kupitia filamu ya The Royal Tour iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na filamu ya Amazing Tanzania, ambazo zimeongeza utambulisho wa nchi na kuvutia watalii pamoja na wawekezaji.
Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2024, Tanzania ilishinda tuzo kadhaa za World Travel Awards zikiwemo Africa’s Leading Destination 2024 na World’s Leading Safari Destination 2024.
Aidha, Hifadhi ya Taifa Serengeti iliendelea kushinda tuzo ya World’s Leading National Park kwa miaka sita mfululizo (2019–2024), huku Mlima Kilimanjaro ukishinda tuzo ya African Leading Tourism Attraction 2024.
Katika tuzo za dunia za mwaka 2025, Tanzania ilishinda vipengele vya World’s Leading Safari Destination na World’s Leading National Park kupitia Serengeti, huku Serengeti Balloon Safaris ikishinda tuzo ya World’s Leading Balloon Ride Operator na Jumeirah Thanda Island kushinda tuzo ya World’s Leading Exclusive Private Island.
Msigwa amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanaimarisha hadhi ya Tanzania kimataifa, kuongeza imani ya watalii na wawekezaji, na kuifanya sekta ya utalii kuendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa taifa.


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...