Katika kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) imejidhatiti kuimarisha matumizi ya mfumo wa kidijitali unaowezesha wateja kuomba maunganisho mapya ya maji kwa urahisi zaidi bila kufika ofisini.
Hatua hiyo inalenga kupunguza usumbufu, kuokoa muda na gharama kwa wateja, sambamba na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma. Kupitia mfumo huo, mteja mpya anaweza kutuma maombi yake akiwa mahali popote, kwa kutumia simu janja, kompyuta au kifaa chochote chenye intaneti.
Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, Bi. Lucy Msigwa, ameeleza kuwa mteja anatakiwa kuingia kwenye tovuti ya huduma.maji.go.tz na kufuata hatua chache zilizoainishwa kwenye mfumo huo hadi kukamilisha ujazaji wa fomu ya maombi. Baada ya hapo, atawasilisha taarifa zake kwa njia ya mtandao na kuanza mchakato wa kupatiwa huduma.
Akisisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia, Kaimu Meneja wa Uendelezaji Miundombinu, Mhandisi Frank Tembi, amesema mfumo huo umeboreshwa ili kuhakikisha maombi yanashughulikiwa kwa haraka na kwa uwazi zaidi. Amebainisha kuwa matumizi ya kidijitali ni sehemu ya mkakati wa mamlaka katika kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na kuboresha huduma kwa jamii.
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mawasiliano kwa Umma, Bw. Juma Mwakaje, amewahimiza wananchi kutembelea pia tovuti ya SOUWASA na kutumia kipengele cha Huduma za Haraka kuchagua Maunganisho Mapya, ambapo watapata maelekezo ya moja kwa moja ya jinsi ya kuwasilisha maombi yao.
SOUWASA imeeleza kuwa Mfumo huo ni dhamira ya taasisi katika kuhakikisha huduma za maji zinawafikia wananchi kwa urahisi, haraka na kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji, Wananchi wametakiwa kuchangamkia fursa hiyo ili kunufaika na huduma bora zinazotolewa kwa njia ya kisasa zaidi.



.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...