Na Mwandishi Wetu — Dar es Salaam, 12 Februari 2026

Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kimeongoza mdahalo wa kitaalamu uliolenga kujadili matumizi ya Akili mnemba (Artificial Intelligence – AI) katika kuboresha utoaji wa huduma za umma na kuongeza ufanisi wa kiutendaji serikalini. Mdahalo huo umefanyika katika Kituo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (Global Learning Section – GLS) cha Chuo hicho, jijini Dar es Salaam, na umefunguliwa rasmi na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Mrope Daudi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Bw. Mrope alisema serikali inaendelea kuhimiza matumizi sahihi ya teknolojia za kisasa kama sehemu ya mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kupunguza gharama za rasilimali fedha na kuongeza uwazi katika taasisi za serikali. Alilipongeza Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa kuandaa mdahalo huo muhimu ambao unatoa jukwaa kwa watumishi wa umma, wataalamu wa teknolojia na wadau wengine kubadilishana uzoefu na maarifa kuhusu matumizi ya Akili mnemba katika kuongeza tija na ufanisi wa kazi.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa matumizi yenye uwiano wa maadili na teknolojia, akibainisha kuwa Akili mnemba inapaswa kusaidia katika utendaji wa kazi bila kuchukua nafasi ya utu wa binadamu.

“Akili mnemba haichukui nafasi ya mtumishi wa umma, bali ni nyenzo ya kumsaidia kutoa huduma bora, zenye ufanisi na huruma kwa wananchi,” alisema Bw. Mrope kwa msisitizo.

Akihitimisha hotuba yake, Bw. Mrope alizitaka taasisi za serikali, hususan zile zinazoshughulika na teknolojia ya habari na mawasiliano, pamoja na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, kuendelea kufanya tafiti na kuibua ubunifu katika matumizi ya teknolojia serikalini. Alisema maoni na mapendekezo yatayotokana na mdahalo huo yatasaidia serikali kuboresha sera na miongozo ya matumizi ya teknolojia kwa kuzingatia DIRA ya Taifa 2050 na mipango ya maendeleo endelevu.

Awali, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho, amesema chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kimejipanga kuhakikisha kinaendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza ubora wa utumishi wa umma kupitia mafunzo, mijadala ya kitaalamu na tafiti za teknolojia. Ameeleza kuwa mjadala wa mwaka huu unalenga kujadili namna Akili Mnemba inavyoweza kuboresha utoaji wa huduma serikalini, kuimarisha maamuzi ya kiutawala na kushughulikia masuala ya maadili bila kuvunja misingi ya mtumishi wa umma.

Mdahalo huo ulimewakutanisha watunga sera, wataalamu wa teknolojia, wanasayansi wa data, wasomi pamoja na wawakilishi kutoka wizara, taasisi, idara na wakala mbalimbali za serikali. Washiriki walijadili ana kwa ana na wengine walishiriki kwa njia ya mtandao, hatua iliyoufanya kuwa mjadala wa kina, shirikishi na wenye tija katika kuimarisha matumizi ya teknolojia ya Akili mnemba ndani ya utumishi wa umma nchini.











 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...