Na Farida Mangube, Morogoro

Wafanyabiashara na walipakodi wa Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji kodi ujulikanao kama IDRAS, unaosimamiwa na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA).

Mafunzo hayo yametolewa na maofisa wa TRA Wilaya ya Kilombero katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, yakilenga kuwajengea uwezo walipakodi juu ya matumizi sahihi ya mfumo huo wa kidijitali.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja wa TRA Wilaya ya Kilombero Innocent Minja, amesema kuwa mfumo wa IDRAS (Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Kodi za Ndani) umeanzishwa kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha TRA inakuwa na mifumo ya kisasa inayosomana na kuunganishwa na taasisi nyingine za serikali.

Mfumo huo ulioanza rasmi Februari 9, 2026, una uwezo wa kuruhusu mifumo mbalimbali ya kiserikali kusomana na kubadilishana taarifa kwa urahisi.

Aliongeza kuwa malengo ya kuanzishwa kwa IDRAS ni kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuimarisha uwazi na usawa katika makadirio ya kodi, kurahisisha ulipaji wa kodi kwa njia ya mtandao, kupunguza muda na gharama ambazo walipakodi walikuwa wanatumia kufuata huduma za ana kwa ana, pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali kupitia mfumo jumuishi unaounganisha taasisi mbalimbali.

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kutumia mfumo huo kwa ufanisi zaidi, kufuatilia malipo yao ya kodi kwa urahisi na kuboresha ushirikiano kati yao na TRA.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za TRA za kuimarisha utendaji wa walipakodi na kuhakikisha mfumo wa kodi unafanya kazi kwa ufanisi zaidi katika mazingira ya kidijitali.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...