WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe.Prof.Adolf Mkenda, amesema kuwa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) , kuna haja kubwa ya kuibua na kulea waandishi bunifu wa Kitanzania ili kuongeza upatikanaji wa vitabu vya ubora vinavyoweza kutumika shuleni na wakati huohuo kuimarisha fasihi ya Kiswahili.

Ameyasema hayo leo Februari 17,2026 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa vitabu Vya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya uandishi bunifu ambapo amesema lengo la Tuzo hizo ni kuongeza idadi ya vitabu vinavyoandikwa na Watanzania na kuhamasisha uandishi wa kibunifu.
"Tuzo hii imepewa jina la Julius Kambarage Nyerere kwa kutambua mchango wake mkubwa katika fasihi ya Kiswahili, Mwl.Nyerere aliandika mashairi na kufasiri kazi za kifalsafa pamoja na tamthilia za Shakespeare kwa vina na mizani sahihi, hivyo kuenzi urithi wake wa kiutamaduni na kielimu,"amesema Prof.Mkenda

Akizungumzia changamoto zinazoikabili Sekta ya uchapishaji, Waziri Mkenda amesema Serikali imeweka mkakati wa kununua na kusambaza vitabu vya washindi wa Tuzo hiyo shuleni na katika maktaba mbalimbali, hatua inayolenga kuhakikisha soko la uhakika kwa wachapishaji na kuongeza faida kwa waandishi. Kupitia mpango huo, uandishi unapata thamani ya kiuchumi na kijamii huku Sekta ya uchapishaji ikipewa fursa ya kukua.

Aidha, Prof. Mkenda amesisitiza umuhimu wa watoto wa Kitanzania kusoma vitabu vya ndani, akieleza kuwa kutegemea vitabu vya nje pekee hakutoshi katika kujenga utambulisho wa kitaifa. Amesema vitabu vinavyoakisi mazingira, historia na tamaduni za Tanzania vinawasaidia watoto kujitambua na kuthamini urithi wao.

Amehitimisha kwa kueleza kuwa uzinduzi wa vitabu vya washindi wa Tuzo hiyo ni hatua muhimu katika kuhifadhi utamaduni, kuimarisha elimu na kuandaa vizazi vijavyo. Tukio hilo, amesema, ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kuwekeza katika elimu, fasihi na kukuza sekta ya uchapishaji nchini.

Kwa uapnde wake Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere, Prof. Penina Mlama, amesema kuwa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu imeongezeka kutoka nyanja mbili za awali riwaya na ushairi hadi kufikia nyanja nne ambazo ni riwaya, ushairi, vitabu vya watoto na tamthilia.

Amesema mwitikio wa waandishi bunifu kushiriki umekuwa mkubwa na ndio maana nyanja hizo zimeongezeka ili kupanua wigo wa waandishi kushiriki.

Profesa Mlama ameeleza kuwa mwaka 2024/2025 washiriki 31 walijitokeza kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani, pamoja na Watanzania walioko nje ya nchi kama Ujerumani, Austria na Czech Republic huku usawa wa kijinsia ukiendelea kuimarika, wanawake wakifikia asilimia 33.3 ya washiriki mwaka 2025.

Akizungumzia muundo wa zawadi, Profesa Mlama amesema washindi hupokea fedha taslimu ambapo mshindi wa kwanza hupata shilingi milioni 10, wa pili milioni 7 na wa tatu milioni 5. Mbali na fedha, mshindi wa kwanza katika kila nyanja hupata muswada wake kuchapishwa na kusambazwa shuleni na maktaba za taifa.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Anneth Komba, amesema kuwa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi bunifu ni nyenzo muhimu ya kuibua na kukuza vipaji vya waandishi wa ndani.

Ameeleza kuwa mpango huo ni chombo cha kitaifa cha kutambua ubunifu na kuendeleza utamaduni wa Kiswahili kupitia maandiko ya waandishi chipukizi na waliobobea.

Dkt. Komba amebainisha kuwa hatua ya kusambaza vitabu kwa shule zote nchini inalenga kuimarisha utamaduni wa kusoma na kuongeza kiwango cha elimu ambapo jumla ya nakala 120,000 za vitabu vitatu vya riwaya Biarasa, ushairi Mgoma ya Mwere, na hadithi za watoto Maziwa ya Kijiji vimechapishwa na vitasambazwa kwa shule.

Ameongeza kuwa kila Shule itapata kati ya vitabu 8 hadi 10. Vitabu hivyo vitatumika kama rasilimali za maktaba na vinatarajiwa kusomwa na wanafunzi wengi, hatua inayoongeza upatikanaji wa maarifa na kuhamasisha kizazi kipya kupenda kusoma.

Amesema kuwa kiasi cha shilingi milioni 100 kilitengwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya uchapishaji na usambazaji. Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha upatikanaji wa vitabu bora na kuimarisha uchumi wa maarifa nchini.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...