Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imetia saini mkataba wa uwekezaji katika sekta ya madini kwa ajili ya kuendeleza leseni ya uchimbaji wa dhahabu katika eneo la Kigosi, mkoani Geita.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa chachu mpya ya kukuza uchumi wa eneo hilo na taifa kwa ujumla.

Hafla ya utiaji saini imefanyika Februari 24, wilayani Bukombe mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa, aliyekuwa mgeni rasmi.

Mkataba huo umehusisha pande mbili ambazo ni STAMICO na kampuni ya Plantcor Mining and Plant Hire PTY Ltd ya Afrika Kusini, ambayo itawekeza katika uendelezaji wa mradi huo wa dhahabu.

Kiruswa ametoa maagizo kwa STAMICO pamoja na mwekezaji kuhakikisha kuwa uwekezaji huo unatekelezwa kwa vitendo na kuanza kazi mara moja bila kupoteza muda, ili uweze kuleta manufaa kwa wananchi wa Kigosi na maeneo jirani.

Aidha, amesisitiza kuwa mradi huo unapaswa kupanua wigo wa shughuli za uchimbaji katika eneo la Kigosi ili kuwapa nafasi wachimbaji kupata maeneo halali ya kuendelea na shughuli zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa STAMICO, Simon Sirro, amewaomba wananchi waliokuwa wakifanya shughuli katika pori la Kigosi kushirikiana na uwekezaji huo mpya na kuepuka kuwa chanzo cha vikwazo, hasa kutokana na mazoea yaliyokuwepo kabla ya mradi kuanza rasmi.

Sambamba na hilo, Naibu Waziri Kiruswa amesisitiza umuhimu wa kampuni mwekezaji kuzingatia masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ili kuhakikisha kuwa jamii zinazozunguka eneo la Kigosi na wilaya ya Bukombe zinanufaika moja kwa moja kupitia miradi ya maendeleo kama vile elimu, afya na miundombinu.

Mkataba huo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa Watanzania, ikiwa ni pamoja na Kuongeza ajira kwa vijana, Kuongeza mapato ya serikali,Kuchochea ukuaji wa uchumi wa vijiji vinavyozunguka Kigosi pamoja na Kukuza sekta ya madini nchini

Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Venance Mwasse, amesema kuwa mradi huo utaanza kwa kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia, uchorongaji na uthibitishaji wa rasilimali.

Aidha, hatua zitakazofuata ni pamoja na upembuzi yakinifu wa kiuchumi, maendeleo ya mgodi, ujenzi wa miundombinu muhimu na usimikaji wa mtambo wa uchenjuaji wa dhahabu.

Uwekezaji huu wa dhahabu katika eneo la Kigosi unaonekana kuwa fursa muhimu kwa maendeleo ya mkoa wa Geita na taifa kwa ujumla. Ushirikiano kati ya serikali, mwekezaji na wananchi utakuwa nguzo kuu ya kuhakikisha mradi huu unaleta matokeo chanya na endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...