Kikundi cha Kinamama Kihesa kilichoanzishwa mwaka 2008 leo kimeadhimisha Siku ya Wapendanao kwa kufanya sherehe ya pamoja na kutembelea Shule ya Viziwi ya Iringa ambapo wametoa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi na walezi wao.
Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa kikundi hicho Upendo Makasi amewashukuru wanachama kwa kuendelea kudumisha umoja na mshikamano tangu kuanzishwa kwa kikundi hicho mwaka 2008.
Amesema kwa miaka yote wamekuwa wakijitoa katika shughuli mbalimbali za kijamii zenye lengo la kusaidia makundi yenye uhitaji maalum.
Ametoa wito kwa jamii kuendelea kujitolea na kusaidia watu wenye changamoto mbalimbali akisisitiza kuwa upendo wa kweli unaonekana kupitia matendo.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Shule ya Viziwi Iringa Abraham Moses amesema shule hiyo inapokea wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania.
Ameeleza kuwa wanafunzi hao wanahitaji upendo na mazingira bora ya kujifunzia ili waweze kutimiza ndoto zao.
Amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 120 kuanzia darasa la kwanza hadi la saba huku muda wa masomo ukitofautiana kulingana na mahitaji maalum ya wanafunzi ambapo baadhi yao huchukua hadi miaka saba au zaidi kukamilisha mzunguko wa elimu ya msingi.
Aidha ametaja changamoto ya afya kuwa ni kubwa akisema wanafunzi wanapougua hukosa huduma za matibabu kwa wakati kutokana na ukosefu wa bima za afya.
Amesisitiza umuhimu wa kupatiwa bima za afya kwa wanafunzi hao ili kupunguza gharama kubwa za matibabu.
Pia ameeleza kuwa shule inakabiliwa na changamoto ya usafiri, kwani gari lililopo ni bovu na haliwezi kutumika ipasavyo wakati wa dharura au shughuli mbalimbali za shule.
Vilevile, amesema kuna baadhi ya wazazi huwapeleka watoto wao shuleni hapo lakini hawarudi tena kuwasalimia wala kuwachukua hali inayosababisha mzigo mkubwa wa malezi na gharama kubaki kwa shule.
Naye Mwakilishi wa Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kihesa Mwl. Grace Sanga, amewashukuru kinamama hao kwa moyo wao wa kujitolea.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kwa jamii na ushiriki wa wadau katika kuongeza nguvu ni jambo la kupongezwa na kuungwa mkono.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...