Na Belinda Joseph-Arusha.
Mwenyekiti wa Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Hamisa H. Kalombola, amesema kuwa usimamizi bora na ushirikishwaji wa maoteo ya bajeti kwa Taasisi za Umma ni nguzo muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wenye ufanisi wa bajeti na mipango ya maendeleo, sambamba na kupunguza migogoro, kudhibiti mianya ya ubadhirifu na kujenga utamaduni wa uwazi na uwajibikaji.
Akizungumza leo Februari 3, 2026, Jijini Arusha, wakati wa ufunguzi as Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Kalombola amesema kuwa usimamizi wa fedha unaozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu huongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali za umma na kuhakikisha fedha zinatumika kwa manufaa ya Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Amesema mkutano huo umeiwezesha Tume kupitia na kujadili Makadirio ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, pamoja na kubainisha vipaumbele vya kimkakati, maeneo yanayohitaji maboresho ya kimfumo na kiutendaji, pamoja na mpango wa matumizi ya bajeti mpya itakayokuwa dira ya utekelezaji wa shughuli za Tume.
Ameeleza uwa bajeti ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa mipango ya Taasisi, kwani huwezesha kupanga, kutekeleza na kutathmini shughuli kwa ufanisi, amesisitiza kuwa mjadala wa bajeti una uzito mkubwa katika kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika kwa uangalifu, weledi na tija.
Ameongeza kuwa kupitia bajeti hiyo, utekelezaji wa mipango, miradi na majukumu ya kila siku ya Tume kwa mwaka ujao wa fedha utaongozwa ipasavyo, huku Tume ikiweza kubainisha vipaumbele vyake, matumizi ya rasilimali na mikakati ya kuboresha utendaji kazi.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma, John C. Mbisso, alisema kuwa bajeti hiyo ndiyo itakayokuwa msingi wa utekelezaji wa mipango, miradi na majukumu ya Tume kwa mwaka ujao wa fedha.
Ameongeza kuwa Tume imeendelea kukua, kuboresha utendaji na kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiutendaji, akibainisha kuwa mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa ni matokeo ya ushirikiano wa wafanyakazi wote kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu.
Mbisso alisisitiza kuwa mikutano ya Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu la kubadilishana mawazo, kufanya tathmini ya pamoja na ukuhakikisha mipango ya matumizi ya fedha za umma inazingatia maslahi mapana ya Taasisi.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...