Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MKUTANO Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji 2026 umeanza rasmi jijini Dodoma kwa mijadala mizito inayolenga kuimarisha sekta ya utangazaji nchini. Mkutano huo wa siku mbili ulioanza leo Februari 12, 2026 unatarajiwa kuhitimishwa kesho Februari 13, 2026.

Mkutano huo umeandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ukishirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya habari wakiwemo wamiliki wa televisheni, redio na majukwaa ya mitandao ya kijamii kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Akiwasilisha mada ya kwanza, Mhandisi Andrew Kisaka kutoka TCRA alizungumzia matokeo na utekelezaji wa mapendekezo yaliyotokana na utafiti wa huduma za utangazaji nchini. Alieleza hatua zilizochukuliwa kuboresha ubora wa maudhui, kuimarisha usimamizi wa leseni pamoja na kuzingatia weledi katika utoaji wa taarifa kwa umma.

Wasilisho la pili lilitolewa na Mhadhiri Msaidizi Zuhura Selemani ambaye alielezea fursa na faida za uwekezaji wa teknolojia katika utangazaji vijijini. Alisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia za kisasa kufikisha taarifa kwa wananchi wa maeneo ya pembezoni na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Nancy Mwaisaka kutoka UNESCO aliwasilisha mada kuhusu TEHAMA na huduma za utangazaji wa redio vijijini, akitoa uzoefu wa taasisi hiyo katika kusaidia redio za kijamii. Alibainisha kuwa redio za vijijini zina mchango mkubwa katika kuelimisha jamii na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Washiriki wa mkutano huo wanatarajiwa kujadili kwa kina changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya utangazaji, huku wakitoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mazingira ya kazi na kulinda maslahi ya umma katika upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...