▪️Benki ya Dunia yafurahishwa na mchango wa Sekta ya Madini wa kuchochea Uchumi Tanzania
📍 Cape town – Afrika Kusini
Sekta ya Madini Tanzania kupitia Kongamano la Mining Indaba 2026 imeendelea kuimarisha nafasi yake kimataifa, huku Tanzania ikiendelea kujidhihirisha kama kimbilio la uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa kuvutia mashirika ya kimataifa, kampuni mbalimbali na wawakilishi wa kidiplomasia.
Februari 10, 2026, Waziri wa Madini alikutana na wadau muhimu ikiwemo Benki ya Dunia katika vikao vya pembeni vya kongamano linaloendelea jijini Cape Town, Afrika Kusini, pamoja na kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Madini wa SADC.
Australia Yaipa Kipaumbele Tanzania Sekta ya Madini
Katika kikao kilichofanyika baina ya ujumbe wa Australia na Tanzania, Naibu Balozi wa Australia Christopher Ellinger alieleza kuvutiwa na mwenendo wa Sekta ya Madini nchini na kusema kwamba kwa kampuni za Australia, Tanzania ni moja ya machaguo ya kwanza kwa uwekezaji. Pia, amesisitiza utayari wa nchi hiyo kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza miradi ya madini kupitia kampuni za Australia, na kuomba ufafanuzi wa Kanuni za Madini za ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta, hasa katika utoaji wa huduma migodini.
Benki ya Dunia yaiweka Tanzania kama Msingi wa Uwekezaji Afrika
Benki ya Dunia imetambua sekta ya madini Tanzania kama eneo la kimkakati lisilopaswa kuachwa pembeni katika juhudi za maendeleo na uwekezaji, ikiashiria uhitaji wa kuendelea kuwekeza na kushirikiana na serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuongeza faida za kiuchumi.
Benki hiyo imeunga mkono mpango wa Tanzania kujiimarisha katika shughuli za utafutaji na utafiti wa rasilimali madini na dhamira ya uongezaji thamani madini ndani ya nchi badala ya kutegemea uzalishaji na usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi. Hii inaonesha umuhimu wa sekta ya madini katika mipango ya maendeleo ya Tanzania na uhusiano wake na wadau wa kimataifa.
Waziri wa Madini alisisiza dhamira ya Serikali kuimarisha ushirikiano wa kufanya tafiti za kina za jiosayansi ambazo zitaongeza wingi wa taarifa na kuchochea uwekezaji nchini. Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza umuhimu wa kipaumbele cha kuongeza thamani madini ndani ya nchi kama njia ya kuongeza manufaa yatokanayo na rasilimali madini badala ya kuuza madini ghafi kwa waongezaji thamani nje ya nchi.
UWEKEZAJI WA FARU GRAPHITE MAHENGE KULETA MAPINDUZI MAKUBWA NCHINI
Waziri wa Madini
Anthony Mavunde, alisisitiza kwamba kaulimbiu ya “Madini ni Maisha na Utajiri” inaweka kipaumbele cha kufanya tafiti za jiosayansi na kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi. Amesema Serikali iko tayari kushirikiana na wawekezaji wote wanaochangia maendeleo ya sekta ya madini nchini kwa kuzingatia Kanuni, Sheria na miongozo iliyowekwa. Aliyasema hayo alipokutana na Kampuni ya Faru Graphite inayomilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na Kampuni ya Black Rock Mining inayotarajia kuchimba madini ya kinywe, katika eneo la Mahenge, Wilayani Ulanga, Mkoani Morogoro. Katika kikao hicho, Kampuni hiyo imetangaza maendeleo mazuri kwenye mradi huo na kuwashukuru viongozi wa Serikali kwa ushirikiano unaowawezesha kufanikisha kazi.
PLANTCOR MINING, STAMICO Mguu Sawa Kuchimba Dhahabu KIGOSI
Katika kikao na Waziri Mavunde, kampuni ya uchimbaji madini na ukodishaji wa vifaa vya uchimbaji ya Plantcor Mining yenye makazi yake nchini Afrika Kusini ambayo ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kusaini Mkataba na Shirika la Madini laTaifa (STAMICO) ilimhakikishia Mhe. Mavunde kwamba mara baada ya kusaini mkataba huo wa ubia na STAMICO itaanza kushirikiana na STAMICO kuendeleza mradi wa uchimbaji madini ya dhahabu kwenye leseni inayomilikiwa na STAMICO katika eneo la Kigosi,Mkoani Geita.
Breakthrough Attorneys na Benki ya NMB washirikiana kuvutia uwekezaji Tanzania
Kampuni ya Breakthrough Attorneys na benki ya NMB, zimeshirikiana kuandaa na kutekeleza warsha ya kuitangaza sekta ya madini na kuvutia uwekezaji nchini Tanzania. Warsha hiyo iliyofanyika Februari 10, 2026 jijini Cape Town nchini Afrika Kusini na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya madini kutoka sehemu mbalimbali duniani. Breakthrough Attorneys ni kampuni ya kisasa ya huduma za kisheria yenye makao yake Tanzania, inayotoa huduma mbalimbali za kisheria za kimataifa kwa kampuni, taasisi za fedha, taasisi za Serikali na watu binafsi.
Akizungumza katika warsha hiyo, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde ambaye alikuwa mgeni rasmi, alieleza kuwa Tanzania inahama kutoka kumiliki rasilimali za madini pekee kwenda kushiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani wa madini. Alisisitiza kuwa uongezaji thamani nchini Tanzania si kikwazo bali ni fursa, na kuwaasa wawekezaji kuitumia fursa hiyo kikamilifu. Alisema kuwa uongezaji thamani madini unaodhamiriwa Tanzania ni ule unaojengwa kupitia ushirikiano, unaoendana na Dira ya Madini ya Afrika (Africa Mining Vision) na sera za viwanda ambazo ni rafiki kwa wawekezaji.
Mhe. Mavunde alipongeza ongezeko la mchango wa taasisi za fedha nchini, akitolea mfano wa Benki ya NMB, ambayo inashirikiana kikamilifu na wawekezaji wa madini katika hatua zote za mnyororo wa thamani na inashiriki kuvutia wawekezaji ndani nan je ya nchi. “Muunganiko kati ya ufadhili wa kifedha wa ndani na wa kimataifa ni ishara muhimu inayoashiria kuwa sekta ya madini ya Tanzania ina uwezo wa kufadhiliwa, kukopesheka, na kuvutia uwekezaji," alisema Waziri Mavunde.




.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...