Na Nasra Ismail, Geita
Wananchi wa Mitaa ya Magogo Ibolelo na 14 Kambarage, Kata ya Buhalahala, Manispaa ya Geita, wamemuomba Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Chacha Wambura, kuwasaidia kufanya ukarabati wa barabara ambazo kwa sasa zimeharibika kwa kiasi kikubwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kutokana na mvua hizo, baadhi ya barabara zimekatika na nyingine kujaa maji, hali inayosababisha adha kubwa kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri na wananchi kwa ujumla.
Kufuatia kilio hicho, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Chacha Wambura, ametembelea maeneo hayo kwa lengo la kujionea hali halisi ya ubovu wa miundombinu hiyo.
Wananchi wametumia fursa hiyo kueleza changamoto wanazokumbana nazo kila siku, zikiwemo kushindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii kutokana na ubovu wa barabara hizo, huku wakimuomba mbunge kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Chacha Wambura, amewatoa hofu wananchi kwa kueleza kuwa tayari hatua stahiki zimeanza kuchukuliwa ili kukabiliana na changamoto zilizolalamikiwa.
Amesema kupitia ushirikiano wa ofisi yake, Ofisi ya Diwani na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), mipango ya matengenezo ya muda na ya kudumu inaendelea.
Wananchi wameonesha matumaini yao kuwa ahadi hiyo itatekelezwa kwa wakati ili kumaliza tatizo hilo ambalo limekuwa likiwakabili kwa muda mrefu.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...