
Harry Kitilya Kamshna Mstaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akizungumza na waandishi wa habari katika sherehe ya wastaafu wa TRA iliyofanyika jijini Dar es Salaam Februari 15, 2026.
Yeremiah Mbagi Katibu wa umoja wa wastaafu, akizungumza na waandishi wa habari katika sherehe ya wastaafu wa TRA ya mwaka 2025 iliyofanyika jijini Dar es Salaam Februari 15, 2026.
Catherine Mkerebe, Mwanachama wa umoja wa wastaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania akizungumza na waandishi wa habari katika sherehe ya mwaka 2025 ya wastaafu wa TRA, iliyofanyika Februari 15, 2026 jijini Dar es Salaam
Lucas Kaigarula mratibu wa sherehe ya mwaka ya wastaafu wa TRA akizungumza na waandishi wa habari katika sherehe hiyo Februari 15, 2026 jijini Dar es Salaam.
UMOJA wa wastaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) umetoa wito kwa wananchi kuendelea kulipa kodi, wakisisitiza kuwa wajibu huo ndio unaowezesha upatikanaji wa huduma muhimu kwa jamii.
Hayo yalisemwa Februari 15, 2026, katika sherehe ya mwaka 2026 iliyofanyika jijini Dar es Salaam, iliyowakutanisha wastaafu hao kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Harry Kitilya, Kamishna Mstaafu wa mamlaka hiyo ambaye alikuwa mgeni wa heshima, alisema kuwa ili serikali itoe huduma za kijamii ni lazima wananchi walipe kodi.
“Serikali ina jukumu la kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Inapofikia maendeleo ya kijamii, serikali inasema ili huduma ziwafikie wananchi wote, ni lazima kuwe na mapato,” alisema.
Aliongeza kuwa ni lazima kutafuta njia za kupata mapato kwa ajili ya kujenga na kuhudumia miundombinu kama barabara, hospitali na sekta ya elimu inayotolewa bure, pamoja na ulinzi wa polisi na mipaka ya nchi.
“Serikali inapata fedha wapi? Kwa hiyo lazima wananchi walipe kodi. Isionekane tu serikali inachukua kodi bila kutoa huduma. Unapolipa kodi ndipo serikali inajenga barabara, shule, hospitali na kuimarisha majeshi yetu yanayotulinda. Hayo ni machache tu,” alisema Kitilya.
Yeremiah Mbagi, Katibu wa umoja huo aliyestaafu kazi TRA mwaka 2019, alisema TRA imeendelea kupiga hatua kubwa ukilinganisha na kipindi walichokuwa wakifanya kazi, hasa katika kuboresha mifumo ya ukusanyaji kodi.
“Huko nyuma tulikuwa tunatumia njia za kizamani, lakini sasa kuna maendeleo. Kuna mifumo mizuri inayoboresha ukusanyaji wa kodi. Napenda kuipongeza serikali na TRA kwa kuendelea kuboresha mifumo,” alisema.
Akizungumzia kuungana kwao, alisema hali ya upweke baada ya kustaafu ndiyo iliyowasababisha kuanzisha umoja huo, kwa kuwa muda mwingi waliutumia kazini.
“Baada ya kufanya kazi zaidi ya miaka 30 au 40, tulipostaafu tulijikuta hatuna watu wa kuongea nao kwa sababu kila mmoja anakuwa na maisha yake. Watu wakaanza kuhisi upweke, tukaona ni vizuri kuungana ili tukutane, kubadilishana mawazo na kufanya shughuli za kijamii, ikiwemo kuwasaidia wasiojiweza,” alisema.
Kwa upande wake, Lucas Kaigarula, mratibu wa shughuli hiyo, alisema sherehe hiyo imelenga kuwakutanisha wastaafu wa TRA ili kuendelea kujadili masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Catherine Mkerebe, mmoja wa wastaafu wa TRA, alisema mamlaka hiyo imeendelea kuboreshwa siku hadi siku na kwamba sasa walipa kodi wamesogezewa huduma karibu zaidi.
“Mifumo ilivyoboreshwa, hata wafanyabiashara wanapata rekodi za mapato yao na kujua faida na hasara,” alisema.
Alisema pia kuwa awali alikuwa na hofu kuhusu maisha ya kustaafu.
“Nilijua nikistaafu nitakuwa na maisha mafupi, lakini sasa naona maisha mazuri,” alisema.
Rose Mahali, mstaafu mwingine, alisema TRA imeongeza usanifu na kuimarisha uhusiano na walipa kodi, na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari.
Aidha, alisema TRA iliwaandaa kuishi maisha baada ya kustaafu.
“Tumefundishwa kwamba kustaafu si mwisho wa kufanya kazi, ndiyo maana wengi wetu hapa tunaendelea kujishughulisha,” alisema.


.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...